Mshambuliaji Cristiano Ronaldo amekubali kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia klabu ya Real Madrid hadi mwaka 2021.

Klabu ya Real Madrid imetangaza kufanikiwa kwa dili hilo, kufuatia kazi kubwa iliyofanywa na rais Florentino Perez, ambaye kwa kiasi kikubwa alichukua jukumu la kuzungumza na nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ureno.

“Ronaldo atasaini mkataba mpya baadae hii leo, na kisha atazungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano Santiago Bernabeu stadium kuanzia saa saba na nusu mchana” imeeleza taarifa iliyotolewa na Real Madrid.

“Mshambuliaji huyo kutoka nchini Ureno atasaini mkataba ambao utamuweka hapa hadi Juni 30-2021, atakua sambamba na rais wa klabu Florentino Perez, katika mkutano na waandishi wa habari.” Imeongeza taarifa hiyo

Ronaldo anakua mchezaji wa pili kukubali kusaini mkataba wa kuendelea kuitumikia Real Madrid, akitanguliwa na Gareth Bale ambaye alifanya hivyo juma lililopita.

Ronaldo mwenye umri wa miaka 31, alijiunga na Real Madrid akitokea Manchester United kwa ada ya uhamisho ya Pauni milioni 80 ambayo iliweka rekodi ya dunia kwa mwaka 2009.

Mpaka sasa ameshaifungia klabu hiyo mabao 350, sambamba na kutwaa ubingwa wa Ulaya mara mbili, ubingwa wa ligi ya Hispania mara mbili, ubingwa wa kombe la Mfalme mara mbili, Supercopa mara mbili, UEFA Super Cup na klabu bingwa duniani (FIFA Club World Cup) mara moja.

Jack Wilshere Arejeshwa Kundini
FBI: Clinton hana kosa la kujibu