Mshambuliaji mpya wa mabingwa wa soka nchini Italia Juventus Cristiano Ronaldo hatokua sehemu ya kikosi kitakachofanya ziara nchini Marekani, kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi.

Uongozi wa klabu ya Juventus umethibitisha mshambuliaji huyo hatoongozana na timu kwenye ziara hiyo, baada ya kumtambulisha katika mkutano na waandishi wa habari mwanzoni mwa juma hili.

Suala la mshambuliaji huyo kutokwenda katika ziara hiyo ya Marekani, limepewa uzito na mkuu wa benchi la ufundi klabuni hapo Massimiliano Allegri, ambapo ameshauri ni bora Ronaldo akasalia Italia, kwa ajili ya mapumziko.

Endapo Ronaldo angejumuishwa kwenye safari ya Marekani, alikua na uwezekano mkubwa wa kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya klabu yake ya zamani Real Madrid, ambao umepangwa kuchezwa August 5.

Makubaliano yaliyofikiwa kati ya uongozi wa juu na benchi la ufundi, yamempa nafasi Ronaldo kuanza rasmi mazoezi Julai 30, tarehe ambayo itakua maalum kwa wachezaji walio mapumziko baada ya fainali za kombe la dunia kurejea klabuni hapo.

Wachezaji wengine ambao wataanza mazoezi Julai 30, Dybala, Douglas Costa, Bentancur, Higuaín na Juan Cuadrado.

Wengine ambao walifika hatua za juu kwenye fainali za kombe la dunia watajiunga na kikosi August 08, ambao ni Mandzukic, Matuidi na Pjaca, huku kikosi kamili kikitarajia kurejea Italia na kuendelea na maandalizi ya msimu August 12.

Katika ziara ya Marekani, Juventus watacheza michezo ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi kupitia michuano ya ICC dhidi ya mabingwa wa Ujerumani FC Bayern Munich mjini Philadelphia Julai 26.

Watacheza dhidi ya Benfica ya Ureno mjini New York Julai 28, kisha watapambana na kikosi maalum kilichoundwa kutoka ligi ya Marekani (MLS All-Star) mjini Atlanta August 2. Na ziara yao itamalizika baada ya mchezo dhidi ya mabingwa wa soka barani Ulaya Real Madrid mjini Washington August 5.

Muna afunguka 'Casto alikataa mimba ikiwa na wiki mbili'
Diamond atoa ofa kuwasafirisha watu 30 Afrika kusini 'Birthday ya Tiffah'

Comments

comments