Mshambuliaji wa klabu ya  Real Madrid, Cristiano Ronaldo ameshinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Kiume wa Mwaka 2017 nchini Ureno.

Ronaldo ametangazwa mshindi wa tuzo hiyo katika tamasha lililofanyika usiku wa jana mjini Lisbon, akiwapiku kiungo wa Manchester City, Bernardo Silva na kipa wa Sporting Lisbon, Rui Patricio, akiwa amepata asilimia 65 ya kura zote, dhidi ya asilimia 18 za Patricio na asilimia 17 za Bernardo.

Mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Ronaldo ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Ureno, amesema anaitoa tuzo hiyo kwa watoto wake.

“Ni tuzo ya wenzangu wote pia, mwaka 2017 ulikuwa mwaka mzuri, usiosahaulika kwa mafanikio ya pamoja na binafsi. Pia naitoa tuzo hiii kwa watoto wangu wanne. Ni rekodi nyingine kwa watoto watatu ndani ya miezi mitatu,” amesema.

Miongoni mwa mambo yaliyochangia kushinda tuzo hiyo ni kuisaidia Real Madrid kushinda taji la La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu wa pili mfululizo mwaka 2017.

Mbali na Ronaldo, kocha wa Monaco, Leonardo Jardim pia ameshinda tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka baada ya kuiongoza timu hiyo ya Ufaransa kushinda taji la Ligue 1 na kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya, wakati kocha wa Manchester United, Jose Mourinho akishinda tuzo ya Vasco da Gama kwa kuitangaza soka ya Ureno.

Magazeti ya ndani na nje ya Tanzania leo Machi 21, 2018
Pierre Lechantre kufumua kikosi mwishoni mwa msimu