Mwanasoka bora barani Ulaya, Cristiano Ronaldo amesifia uwezo wa ufundishaji wa meneja wa klabu ya Real Madrid Zinedine Zidane, ambaye alichukua nafasi ya Rafael Benitez baada ya kuonyeshwa mlango wa kutokea mwanzoni mwa mwaka huu.

Ronaldo amesifia uwezo wa gwiji huyo wa soka kutoka nchini Ufaransa, kufuatia mwenendo wa mabadiliko aliyoyaona tangu alipokabidhiwa jahazi mwezi Januari.

Ronaldo amesema Zidane ni meneja wa aina tofauti, kutokana na juhudi za ufundishaji wake nje na ndani ya uwanja, jambo ambalo anaamini lilikua chachu ya kutwaa ubingwa wa barani Ulaya msimu uliopita dhidi ya mahasimu wao wa mjini Madrid Atletico Madrid, kwa changamoto ya mikwaju ya Penati.

Lingine ambalo amelizungumza Ronaldo na kufikia hatua ya kuona Zidane ni meneja wenye hadhi ya kupewa sifa, ni hatua ya kukiongoza kikosi cha Real Madrid katika mshike mshike wa ligi kuu msimu uliopita, hadi kufikia hatua ya kumaliza katika nafasi ya pili kwa tofauti ya point moja dhidi ya FC Barcelona, jambo ambalo lilikua halitarajiwi na mashabiki wengi duniani.

“Zidane alikua msukumo mkubwa wa mafanikio tuliyoyapata msimu uliopita,”

“Alileta utofauti mkubwa kikosini tangu siku ya kwanza alipoanza kazi hadi tulipofikia mwisho wa msimu, alifanya kazi wakati wote na kutuhamasisha kucheza kwa kujituma bila kuhofia mbinu za mpinzani yoyote tuliyekutana nae. ”

“Kwa mawazo yangu, Ninaamini Zindane ni mtu wa kipekee na ninamuweka katika hadhi ya mameneja wakubwa ambao nimewahi kufanya nao kazi tangu nilipoanza kucheza soka. ”

“Zidane anastahili pongezi za kipekee, na ninaamini hata dunia inaliona jambo hilo.” Alisema Ronaldo

Arsenal, Man City Zilipambana Kumsajili Zlatan Ibrahimovic
Khedira: Schweinsteiger Hastahili Kutendewa Hivi