Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewaonya watumishi wa umma walioko Pemba kutojihusisha na masuala ya uvunjifu wa Sheria na taratibu za utumishi wa umma, baada ya kubaini kuwa baadhi yao hufanya ‘vituko’ wakidai kutoitambua Serikali iliyoko madarakani.

Akichangia katika Baraza la Wawakilishi kuhusu bajeti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara Maalum, Waziri asiye na Wizara Maalum, Said Soud Said alisema kuwa wafanyakazi wanaofanya vitendo hivyo wanataka kutumbuliwa majipu.

“Wapo watendaji kule Pemba wanahitaji kutumbuliwa majipu kwa sababu wanajidai kwamba hawajapata Serikali wanayoitaka,” alisema Said. “Serikali hii ya rais Dk Ali Mohamed Shein imechaguliwa kihalali kwa mujibu wa katiba,” aliongeza.

Aidha, alisema kuwa CUF wamekuwa wakifikiria kuwa Serikali ya Dk. Shein haiwezi kuleta maendeleo bila wao, mtazamo ambao aliukosoa vikali.

“Mimi nawaambia wananchi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo madarakani chini ya Rais Shein na inatekeleza majukumu yake vizuri. Hawa CUF wanatakiwa kutambua kwamba hawana hatimiliki ya Zanzibar kwamba sio kweli kuwa kama hawamo serikalini basi hakuna kitakachofanyika.”

Said Soud Said ni Mwakilishi wa kuteuliwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha upinzani cha AFP.

Video: Simu yako itazimwa na TCRA? Tigo wanakuarika ukajipatie simu ya Buree...
Video: Wanajeshi Chad Kupambana na Boko Haram Niger, 4 Wauawa Katika Shambulizi