Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad anatarajiwa kurejea leo kutoka ughaibuni alikoenda kwa ziara ya takribani wiki tatu huku jeshi la polisi likijiandaa kumfikisha Mahakamani.

Hivi karibuni, Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu alieleza kuwa Jarida la Mashtaka dhidi ya Maalim Seif liko kwa Mkurugenzi wa Mashtaka wa Zanzibar, kutokana na kile alichodai kuwa aliwachochea wafuasi wake kufanya fujo kupitia vikao vya ndani vya chama hicho.

IGP Mangu alieleza kuwa uchaguzi wa Oktoba 25 na ule wa Marudio vilifanyika kwa amani na utulivu lakini matatizo na vitendo vya uvunjifu wa amani vilianza kuonekana tangu mwanasiasa huyo aliyegombea Urais kuanza kufanya mikutano hiyo ya ndani akiwahamasisha wafuasi wake kutoshirikiana na Serikali iliyopo madarakani.

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdani Makame amethibitisha kuwa tayari jalada hilo liko kwa DPP na kwamba upelelezi unaendelea.

Akizungumzia mpango huo wa Jeshi la Polisi, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF, Shemeji Mketo aliwaambia waandishi wa habari kuwa chama hicho kimekuwa kikisubiri polisi watekeleze azimio lao hilo ndipo wataeleza msimamo wao.

“Acha wamkamate na sisi tunalisubiri hilo… wakimkamata ndipo tutasema nini tunafanya,” alisema Mketo.

Aidha, Mketo alisema kuwa Maalim Seif atakapowasili atazungumza na waandishi wa habari kuelezea kuhusu ziara yake, nchi alizokwenda na mambo aliyoyafanya.

Video: Shirika la nyumba la taifa latajwa kuchangia uchafuzi wa mazingira
Rafa Benitez Akubali Yaishe, Amfungulia Milango Moussa Sissoko