Baraza Kuu la Chama Cha Wananchi (CUF), jana lilifikia maamuzi ya kumfukuza uanachama Profesa Ibrahim Lipumba kwa madai ya kuvunja katiba ya chama hicho.

Profesa Lipumba ambaye alijiuzulu uenyekiti wa chama hicho mwaka jana na baadae kutengua uamuzi wake mwaka huu, ameendelea kudai kuwa ndiye mwenyekiti halali wa CUF hasa baada ya kupokea barua kutoka kwa Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kuhusu ushauri wake juu ya mgogoro huo.

Mkutano wa Baraza Kuu la CUF

Mkutano wa Baraza Kuu la CUF

Katika kikao chake kilichofanyika jana visiwani Zanzibar, Baraza Kuu la CUF limeeleza kuwa limepitia taratibu zote za kikanuni na kikatiba kufikia uamuzi wa kumfukuza uanachama Profesa Lipumba.

Pamoja na mambo mengine, Baraza hilo limesema kuwa Profesa Lipumba alifanya kosa la kutumia wahuni kuvunja ofisi za Makao Makuu ya chama hicho, Buguruni jijini Dar es Salaam na kuwapiga walinzi halali wa ofisi hizo.

“Kwa maamuzi haya, Baraza Kuu linaweka bayana kwa wanachama wa CUF, Watanzania na mamlaka zote nchini kwamba kuanzia tarehe ya leo, Prof. Ibrahim Lipumba hana haki ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na shughuli zozote za Chama,” limeeleza Baraza hilo.

Kabla ya kufikia uamuzi huo, Baraza hilo lilieleza kuwa limekuwa likimuita Profesa Lipumba kwenye vikao vyake hata kabla ya kumsimamisha uanachama lakini amekuwa akikaidi makusudi kuhudhuria na kujitetea.

Katika hatua nyingine, Baraza hilo limekataa kufuata ushauri wa Msajili wa vyama vya siasa kuhusu mgogoro wa Profesa Lipumba wakieleza kuwa msajili huyo hana Mamlaka kisheria kuingilia masuala ya ndani ya chama.

Hata hivyo, Profesa Lipumba ameeleza kutoyatambua maamuzi hayo kwa madai kuwa kikao kile sio halali.

Rais wa Zamani wa Israel, Shimon Peres afariki
Mwandishi wa Habari Auawa kwa risasi Nchini Somalia, Umoja wa Mataifa Watoa Ripoti yake