Chama Cha Wananchi (CUF) kimewatangazia rasmi wanachama wake na Watanzania kwa ujumla kuwa hakitoshiriki katika uchaguzi mdogo wa marudio katika Kata 79 na majimbo 2 uliopangwa kufanyika nchini kote Tarehe 12 August, 2018.

Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Habari, Uenenzi, Uhusiano na Umma, Mbarala Maharagande kufuatia uamuzi uliotolewa na Kamati ya Utendaji ya Taifa ya CUF mara baada ya kufanya uchambuzi wa kina na tathmini pana juu ya taarifa ya kufanyika kwa uchaguzi huo na kubainisha sababu nyingi zilizopelekea kusitisha ushiriki wao katika uchaguzo huo mdogo wa marudio.

Sababu mojawapo ni uwepo wa mkanganyiko wa uongozi katika usimamizi wa uchaguzi huo uliojitokeza kutokana na Mgogoro uliopandikizwa ndani ya CUF na Lipumba na washirika wake.

Hivyo CUF inaona ni busara kwa sasa kuelekeza nguvu na rasilimali zake chache zilizopo katika kushughulikia na kuupatia ufumbuzi Mgogoro huu uliopandikizwa.

Aidha CUF Imetoa wito kwa Vyama rafiki vyote katika UKAWA kukaa pamoja kufikia muafaka na maridhiano na kusimamisha Wagombea bora, Imara, na madhubuti kugombea nafasi hizo zote.

Pia imetoa wito kwa Viongozi na wanachama wake wote katika maeneo yote ya marejeo ya Uchaguzi kwa Tanzania Bara kushirikiana bega kwa bega kuunganisha nguvu za pamoja na Vyama rafiki vya UKAWA katika uchaguzi huu ili kuishinda CCM.

Aidha Katika kata 79 zilizotangazwa, CUF imepoteza Kata 4 ilizokuwa inaziongoza kwa Madiwani wake kuamia CCM Kata mbili zipo manispaa ya Jiji la Tanga Mjini na Kata moja Mtwara Vijijini na Diwani mmoja Kufariki kutoka Wilaya ya Kwimba.

Kutokana na vigezo vya kitaalamu na kitakwimu na Ramani ya maeneo utakapofanyika Uchaguzi huu wa marudio CUF ingeweza kushiriki kikamilifu katika Kata za Mkakati 11.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza kufanyika kwa uchaguzi mdogo katika Jimbo la Buyungu, mkoani Kigoma ambalo lilikuwa linaongozwa na Mbunge wa Chadema aliyefariki dunia hivi karibuni na kwenye Kata 79 za Tanzania Bara.

Hivyo uchaguzi huo mdogo utafanyika ndani ya halmashauri 43 zilizopo kwenye mikoa 24 ya Tanzania Bara.Mikoa hiyo ni pamoja na, Kigoma, Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Kagera, Katavi, Kilimanjaro, Lindi, Manyara, Mara, Mbeya, Mtwara, Morogoro, Mwanza, Njombe, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Singida, Songwe, Tabora na Tanga.

Kwa upande wa Halmashauri zitakazokuwa na Uchaguzi ni Moshi, Ruangwa, Mbulu, Hanang, Babati, Serengeti, Tarime, Kyela, Mtwara, Newala, Kilombero, Kilosa, Kwimba, Makete, Wanging’ombe na Kalambo.

Pia Songea, Msalala, Meatu, Singida, Songwe, Tunduma, Tabora, Nzega, Urambo, Tanga, Karatu, Longido, Arusha, Ngorongoro, Monduli, Meru, Ubungo, Kondoa, Mpwapwa, Chamwino, Iringa, Kyerwa, Misenyi, Muleba, Nsimbo, Kasulu na Same.

 

Video: Serikali ya awamu ya tano hatuna biashara ya kununua madeni - Majaliwa
Ndege ya Boeing 787-8 Dreamliner kutua leo mchana

Comments

comments