Katika hali isiyo ya kawaida, mfanyakazi wa ndani maarufu kama ‘dada’ anatuhumiwa kuiba mtoto wa miezi miwili wa mwajiri wake mkoani Singida akiwa na lengo la kumdanganya mumewe kuwa amejifungua.

Kwa mujibu wa mama wa mtoto huyo, Hawa Rogers alimuacha nyumbani mtoto wake William akiwa na dada huyo aliyetambulika kwa jina la Habiba Abubakari, lakini aliporejea hakumkuta mtu yeyote.

Ameeleza kuwa baada ya kutoa taarifa polisi, jeshi hilo lilianza kumsaka na hatimaye kumkamata akiwa nyumbani kwao mtaa wa Nyasubi, wilayani Kahama mkoani Shinyanga

Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, Simon Haule amesema kuwa walifanikiwa kumkamata Habida baada ya kupata taarifa kutoka  kwa jeshi la polisi mkoa wa Singida.

Ameeleza kuwa jeshi hilo lilifanya msako hadi nyumbani kwao Habiba na kumkuta akiwa na kichanga huyo.

Baada ya kumhoji, Kamanda Haule amesema kuwa Habiba alikiri kufanya wizi huo akidai kuwa alitaka kumthibitishia mumewe aliyemuacha kwa sababu ya ugumba kuwa hana tatizo hilo tena.

“Alikiri kumuiba mtoto huyo kwa madai kuwa ana tatizo la ugumba lililosababisha aachane na mume wake, kwahiyo alifanya hivyo ili kumuonesha mumewe huyo kuwa ameweza kujifungua,” Kamanda Haule anakaririwa.

Habiba atasafirishwa kurejea mkoani Singida ambako ndiko kesi yake imefunguliwa, kwa ajili ya kujibu mashtaka yanayomkabili.

Video: 'House Girl' matatani kuiba kichanga cha bosi wake, DC atimuliwa kazi akiwa ziarani na Waziri Mkuu
Obama amaliza mapumziko Tanzania na kuwasili Kenya

Comments

comments