KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imejiwekea malengo ya kupambana kuhakikisha inashinda mechi mbili zijazo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya African Sports na Mgambo JKT (sawa na dakika 180) ili kuendelea kusalia kileleni mwa ligi.

Azam FC mpaka sasa imejikusanyia jumla ya pointi 35 ikiwa kileleni kwenye msimamo baada ya kushinda mechi 11, sare mbili na haijapoteza mchezo hata mmoja, inafuatiwa na Yanga iliyofikisha 33, huku Simba na Mtibwa Sugar zikijongea zote zikiwa zimevuna pointi 27.

Katika muendelezo wa ligi hiyo, Azam FC itaanza kwa kucheza na African Sports kwenye Uwanja wa Azam Complex Januari 16 mwaka huu kabla ya kusafiri hadi mkoani Tanga kukipiga na Mgambo JKT ya huko Januari 23, mwaka huu.

Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya jana jioni, Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alisema kuwa ameandaa programu ya siku nne ya mazoezi ya ufiti kwa wachezaji wake kuanzia leo kabla ya kuhamia kwenye yale ya mbinu siku nne au tano za mwisho kabla ya kuvaana na African Sports.

“Tunafanya kazi kwa nguvu sana hivi sasa, ili kuonyesha kiwango kizuri dhidi ya African Sports, tunataka kumaliza raundi ya kwana ya ligi tukiwa bado namba moja hivyo lazima tushinde dhidi ya timu hiyo na ile ya African Sports,” alisema.

Hall alisema kuwa anataka kuimarisha zaidi kiwango cha wachezaji wake baada ya kutocheza vizuri kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, waliyoaga Alhamisi iliyopita kufuatia kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar.

“Tunatakiwa kuwa makini kwenye mazoezi na kufanya mazoezi kwa nguvu ili kurejea kwenye kiwango chetu na ubora wetu, ambao ulipotea Zanzibar, ni mechi moja tu dhidi ya Yanga, ambayo tulicheza kwenye ubora wetu na mechi mbili nyingine tukashindwa,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Zanzibar Heroes na Sofapaka ya Kenya, alisema kiwango kibaya walichoonyesha huko kwa kiasi fulani kimechangia kutotoa mapumziko kwa wachezaji wake mara baada ya kurejea jijini Dar es Salaam Ijumaa hii wakitokea kwenye michuano hiyo, yote hayo akitaka kuwarejeshea makali yao.

“Hivyo kwa sasa tunatilia mkazo zaidi kwenye Ligi Kuu ya Vodacom, lakini pia bado tunatakiwa kuhakikisha tunashindana kwenye michuano mingine, na ndio maana tunafanya mazoezi kwa nguvu kwa ajili mechi dhidi ya African Sports na Mgambo JKT,” alisema.

Alichokiona Mapinduzi Cup

Hall aliyeipa Azam FC taji la Kombe la Kagame Agosti mwaka jana, alisema kuwa amegundua ya kuwa wachezaji wake walikuwa hawana tamaa ya kutosha ya kushinda taji la michuano ya Kombe la Mapinduzi, licha ya kukifanyia mabadiliko kikosi chake mara kwa mara.

“Walikuwa wakifikiria kuwa Kombe la Mapinduzi ni dogo, hivyo haijalishi na hawakuweka malengo katika hilo, wanajua ya kuwa Ligi Kuu ya Vodacom ni muhimu, Kombe la Kagame ni muhimu, Kombe la Shirikisho Afrika ni muhimu, hata pia Kombe la FA ni muhimu kuliko Mapinduzi kwa kuwa bingwa wake atashiriki Kombe la Shirikisho,” alisema.

Aliongeza kuwa: “Kwanza nilienda na malengo ya kuwapa nafasi ya kucheza wachezaji waliokuwa hawapati nafasi ya kucheza ili waonekane na kuwaweka tayari, hii ilitokana na wachezaji wangu kama Wawa (Pascal), Kapombe (Shomari) kuwa na majeraha madogo, hivyo nilitaka kuwa mwangalifu kutokana na hali zao.”

Newcaste United Wamnyatia Jonjo Shelvey
Elimu Bure Yaanza Rasmi, Msako Wa wanaowapa Mimba Wanafunzi Waanza