Jeshi la Polisi mkoani Katavi, linamshikilia mganga mfawidhi wa kituo cha Afya Inyonga wilayani mpanda, Calvin Mnaso (37) kwa tuhuma za kuiba dawa za binadamu pamoja na vifaa tiba katika kituo hicho.

Kamanda wa polisi mkoa wa Katavi, Benjamin Kuzaga ametoa taarifa jana kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Desemba 19, baada ya polisi kupata taarifa za wizi katika kituo hicho.

Amesema baada ya taarifa hizo jeshi la polisi walianza kupekua katika nyumba za baadhi ya watu waliohisiwa kuhusika na wizi huo wakiwemo baadhi ya watumishi wa kituo hicho cha afya.

Kamanda Kuzaga amesema walipofika nyumbani kwa mtuhumiwa na kufanya upekuzi walifanikiwa kukamata mabox matano ya dawa mbalimbali za binadamu, vifaa vya kupima maradhi ya binadamu, vifaa vya kufanyia oparesheni na tohara, godoro moja pamoja na sindano ambavyo vyote ni mali ya serikali.

Hadi sasa mtuhumiwa huyo bado anashikiliwa na polisi na upelelezi ukikamilika anatarajiwa kufikishwa Mahakamani kwa mujibu wa sheria.

Watalii 150 kutoka Israel wametua nchini
Arteta aanza na 'mabavu' Arsenal