Mwenyekiti wa zamani wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, Hassan Dalali amefichua siri ya kufanya maamuzi ya kujitosa kuwania nafasi ya uenyekiti ndani ya klabu hiyo.

Dalali amesema, ameamua kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo kutokana na kukidhi vigezo, na ni haki yake kisheria kutokana na kanuni ya TFF ambayo inaruhusu mgombea mwenye elimu kuanzia kidato cha nne.

Pia ameweka wazi namna alivyopata msukumo kutoka kwa wanachama zaidi ya 50 ambao walimfuata na kumtaka kuwania nafasi ya uenyekiti wa ndani.

“Nimechukua fomu jana kutokana na wanachama kunifuata nyumbani kwangu kuhitaji nifanye hivyo ambao wamenichangia fedha ya kwenda kuchukulia fomu kiasi cha shilingi milioni moja (1,000,000).

“Haina shida iwapo mimi nilikuwa mwenyekiti awali kwa kuwa sikuongoza miaka nane mfululizo, kikanuni inaeleza kuwa iwapo umekuwa mwenyekiti kwa muda wa miaka minne kisha ukaishia hapo na ukakaa pembeni na ukihitaji kugombea tena unaruhusiwa,”

“Nisingeweza kuruhusiwa kugombea iwapo ningekuwa nimeongoza kwa miaka nane mfululizo, kipindi kile sikuweza kugombea kutokana na vigezo vilivyowekwa vya elimu ya digrii lakini sasa uchaguzi unakwenda kwa mujibu wa kanuni ya TFF ambayo inaruhusu mtu kugombea akiwa na elimu ya kidato cha nne,” amesema Dalali.

Kamati ya Uchaguzi ya Klabu ya Simba, imetangaza uchaguzi mdogo ndani ya klabu hiyo kwa ajili ya kuziba nafasi ya aliyekuwa mwenyekiti, Swedi Mkwabi aliyeachia madaraka Septemba, mwaka jana ambapo nafasi hiyo ilikaimiwa na mjumbe wa kamati ya Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mwina Kaduguda.

Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Februari 7 mwakani ambapo zoezi la uchukuaji fomu limeanza Desemba 14 na litafungwa Desemba 24 huku wajumbe watatu wakijitokeza kuchukua fomu hizo.

JPM aitaka tume ya maadili kukaa chonjo na mtandao
Yondani aibukia Polisi Tanzania