Mabingwa wa soka nchini Italia Juventus FC wamekubali kuachana na mlinzi wa kulia kutoka nchini Brazil, Dani Alves ili akatimize ndoto ya kuungana kwa mara nyingine na meneja wake wa zamani Pep Guardiola ambaye kwa sasa anakinoa kikosi cha Manchester City.

Juventus FC wamefikia uamuzi huo, baada ya Alves kuomba kuondoka mjini Turin, licha ya kusaliwa na mkataba wa mwaka mmoja wa kuitumikia miamba hiyo soka nchini Italia.

Alves mwenye umri wa miaka 34, alijiunga na Juventus mwezi Julai mwaka jana akitokea FC Barcelona kwa mkataba wa miaka miwili wenye kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi, lakini ameamua kuibadilikia klabu hiyo ili akaungane tena na Guardiola aliyewahi kufanya nae kazi kwa miaka minne.

Taarifa za awali zinasema tayari Alves alishakubali kujiunga na Manchester City kwa mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Pauni Milioni 8.6.

Bado haijafahamika kama Juventus itataka fidia kutoka na kubariki kuondoka kwa Alves ama itaamua kumwachia huru mlinzi huyo, ikiwa tu ataamua kusamehe mishahara yake yote aliyopaswa kulipwa kwenye mkataba wake uliosalia.

Ikiwa uhamisho huo utakamilika Alves atakuwa mchezaji wa tatu kujiunga na Manchester City tangu kufungiliwa kwa dirisha la usajili barani Ulaya, akitanguliwa na kiungo Bernardo Silva aliyetokea AS Monaco na mlinda mlango Ederson Moraes aliyetokea SL Benfica.

Guardiola anataka kukamilisha usajili wa nyota wapya kabla ya kuanza kwa ziara ya kujiandaa na msimu mpya, ili apate muda wa kutosha wa kukinoa kikosi chake ambacho kilishindwa kutwaa taji lolote msimu uliopita.

?Live: Hotuba ya Rais Magufuli katika uzinduzi barabara ya Bagamoyo - Msata
Taifa Stars Yaenda Afrika Kusini