Beki mpya wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Daniel Amoah, leo Ijumaa ameanza rasmi mazoezi akijiweka sawa na mechi zijazo za timu hiyo.

Amoah aliyesajiliwa mwanzoni mwa mwezi huu akitoka Medeama ya Ghana, aliwasili nchini Jumanne iliyopita mara baada ya kuweka mambo yote sawa nchini kwao huko.

Beki huyo katika majukumu ndani ya timu yake hiyo mpya, atakuwa akitumia jezi namba tatu mgongoni iliyokuwa ikitumiwa na kipa Ivo Mapunda aliyesitishiwa mkataba mwishoni mwa msimu uliopita.

Kuwasili kwa Amoah kunazidi kukiimarisha kikosi cha Azam FC katika idara ya ulinzi hasa baada ya kutokuwa kikosini kwa mabeki wa kati Aggrey Morris na Pascal Wawa, ambao wako kwenye programu ya mwisho ya kutibu majeraha yao ya goti.

Moja ya sifa kubwa za Amoah ni uwezo kukabiliana na washambuliaji wasumbufu akitumia akili na nguvu, ambapo ni mmoja wa wachezaji waliochangia mafanikio ya Medeama kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho mwaka huu.

Beki mwenye umri wa miaka 18, pia ana uwezo wa kufunga mabao ambapo mpaka sasa ameifungia mabao matatu Medeama, kwenye Ligi Kuu ya Ghana akifunga mawili na moja katika Kombe la Shirikisho.

Stand United FC Yang'ang'ana Na Ndoa Iliyovunjika
Mamadou Sakho Amalizana Na Klopp, Asajiliwa Kikosi cha PL