Mtu mmoja anayedhaniwa kuwa ni jambazi ameuawa akijaribu kumpora paroko wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Theresa iliyoko Mbezi jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Ulinzi ya Jatu, Jacobo Mgwabati amewaeleza waandishi wa habari tukio hilo lilivyotokea, Jana, Septemba 6, 2019.

Ameeleza kuwa katika tukio hilo la uporaji, watuhumiwa walikuwa wawili na wote walikuwa na bastola. Alisema walimfuatilia Paroko akitokea benki na alipofika eneo hilo walimbananisha wakimlazimisha awape begi ambalo hata hivyo halikuwa na fedha.

Alisema kuwa watu hao walikuwa na pikipiki na walimuweka katikati Paroko huyo wakitishia kumuua.

“Paroko akaamua kuwapa begi baada ya kumtishia kumpiga risasi. Askari wetu akatumia busara, akaacha paroko asogee mbali nao kwanza, walipoondoka akawafyatulia risasi, moja ikampata mmoja wao kwenye kiuno akaanguka. Hakukaa sana akapoteza maisha na mwingine akakimbia kwa miguu,” Mgwabati anakaririwa na Mwananchi.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Mussa Taibu amemsifu mlinzi wa kampuni ya Jatu kwa kazi aliyoifanya kupambana na waporaji.

Kamanda Taibu amesema kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na wanamtafuta mtuhumiwa aliyekimbia.

Video: JPM amtaka Museveni amtumbue kigogo, Dunia yamlilia shujaa Mugabe
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Septemba 7, 2019