Mohamed Mohamed, mkazi wa jiji la Dar es Salaam amefikishwa mahakamani kwa kosa la kugushi na kuwa na mihuri 54 ikiwa ni pamoja na mihuri ya Ikulu, Mahakama Kuu, Wizara nyeti, Polisi na makanisa mbalimbali nchini.

Mtu huyo amesomewa mashtaka 115 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kiusut Jijini Dar es Salaam, ambapo kati ya mashtaka hayo yapo makosa ya kugushi, kukutwa na mihuri, hati za kusafiria na nyaraka nyingine za kugushi za Serikali.

Katika kesi hiyo iliyofikishwa mbele  ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage, wakili wa Serikali, Paul Kadushi akisaidia na Wankyo Simon alisema kuwa mtuhumiwa alikutwa akitenda makosa hayo kati ya mwaka 2014 na mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti huku akifahamu kuwa ni kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa Wakili Kadushi, mihuri aliyokutwa nayo mtu huyo mbali na ile ya Ikulu na Mahakama Kuu ya Tanzania na Zanzibar ni pamoja na mihuri ya vituo vya polisi, hospitali za rufaa, mawakili, Msajili wa Ndoa, kampuni za bima pamoja na TRA.

Mingine ni ya Makatibu Wakuu wa wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara ya Mambo ya Nje.  Pia, alikutwa na mihuri ya kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania (KKKT), Kanisa Katoliki, Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) na mingine.

Hata hivyo, Mshitakiwa alikana mashtaka yote. Hakimu aliahirisha kesi hiyo baada ya wakili wa Kadushi kueleza kuwa upelelezi unaendelea na hakimu aliitaja Agosti 31 kuwa siku ya kusikiliza tena kesi hiyo.

Video Mpya: Mo Music - Ado Ado
Mabasi 165 ya Mwendo Kasi kununuliwa Dar