Mwaka 2017 ulikuwa mwaka wenye matukio mengi na ulioshuhudia muziki wa kizazi kipya ukipiga hatua kubwa hasa kwenye majukwaa ya kimataifa.

Kwa bahati mbaya, hakukuwa na tuzo maalum ambazo zingetolewa kwa wasanii, hivyo tumeamua kuweka picha ya tuzo za muziki kwa mwaka huo kwa maoni na vigezo ambavyo bila shaka vingetumika kutoa tuzo hizo.

Dar24 tumeamua kuiweka orodha hii leo ili kuipa nafasi juzi ambayo huenda ingekuwa na kitu kingine kikubwa cha kufungia mwaka.

Hii ni orodha kamili ya maoni:

 Wimbo Bora wa mwaka

Seduce Me – Ali Kiba

Seduce Me ilistahili kupata tuzo hii kutokana na ukubwa wake na jinsi ambavyo iligeuka kuwa ‘Wimbo wa Taifa la Bongo Fleva’ ndani ya muda mfupi. Karibu kila mtu aliiongelea Seduce Me, kuanzia wanamuziki, watu wa kawaida hadi viongozi wa Serikali.

Wimbo huu pia uliweka rekodi mpya kwa kuwa wimbo ulioangaliwa mara nyingi zaidi kwenye YouTube ndani ya kipindi cha wiki mbili ukivuta mamilioni ya watazamaji.

Imemaliza mwaka ikiwa imeangaliwa zaidi ya mara Milioni 8.  

Wimbo Bora wa Rap/Hip hop

Fresh – Fid Q

Ngosha aliendeleza ubabe wa uandishi wa mashairi kwenye wimbo huu ambao ni wimbo halisi wa ‘hip hop’. Fresh inastahili tuzo hii katikati ya nyimbo nyingi nzuri za hip hop kwa utunzi, utayarishaji na uwasilishaji wake.

 Wimbo bora wa kuimba

Halleluyah – Diamond feat. Morgan Heritage

Halleluya ni moja kati ya nyimbo mbili nzito zaidi zilizowahi kutolewa na Diamond Platinumz. Wimbo huu unastahili kuwa wimbo bora wa kuimba kwa jinsi uimbaji wake ulikuwa wa kutukuka kuanzia kwa Diamond na Morgan Heritage wenyewe.

Video ya wimbo huu ilivunja rekodi ya Afrika kwenye mtandao wa YouTube, rekodi iliyokuwa inashikiliwa na ‘Closer’ ya Wizkid wa Nigeria aliyemshirikisha Drake. ‘Closer’ iliweka rekodi ya kuvuta watazamaji milioni moja na nusu baada ya saa 24. Halleluyah ilipata watazamaji hao ndani ya saa 15, na ndani ya saa 24 ilikuwa imetazamwa zaidi ya mara milioni mbili.

Ilifunga mwaka ikiwa imeangaliwa zaidi ya mara milioni 8 kwenye mtandao wa YouTube.

 Msanii Bora wa Kike

Vanessa Mdee

Venessa Mdee anastahili tuzo hii kwa jinsi alivyoweza kufanya muziki wake kuwa mkubwa zaidi ndani ya Mwaka na kufanikiwa kupata dili kubwa la kuwa chini ya lebo ya Universal Music, dili ambalo kwa mujibu wake amepewa ‘mkwanja mreeeefu sana’.

Vee Money alifanya nyimbo nyingi kubwa akiwashirikisha wasanii wa ndani na nje ya nchi. Kolabo yake na msanii wa P Square ‘Kisela’ ilimaliza mwaka vizuri zaidi ikizidi kumpa mashavu makubwa.

Ijumaa ya Disemba 29, alifanya ‘Listening Party’ ya albam yake mpya ‘The Money Mondays’ ambayo ni moto wa kuotea mbali tena ukiwa na baridi kali. 

Msanii Bora wa Kiume

Diamond Platinumz

Bado Diamond yule, Boss wa WCB anayejiita ‘Simba’. Ameendelea kuwa msanii aghali kuliko wote nchini, mwenye nyimbo nyingi na kubwa. Mwaka jana alitangaza ujio wa albam yake ‘A Kid From Tandale’ ambayo imepata mashavu ya wasanii wengi wakubwa wa Marekani kama Rick Ross, Neyo na Omarion.

 

Kundi Bora la Muziki – Weusi

Kundi la Weusi lenye wasanii wanNe ambao ni Joh Makini, Nikki wa Pili, G-Nako na Bonta ambalo linajiendesha kwa muundo wa Kampuni, lingeweza kunyakua tuzo hii. Kwanza, limekuwa kundi imara lisiloyumba kwa kipindi chote cha mwaka. Pili, limeachia nyimbo nyingi (Back to back) na zote kubwa huku wasanii wake mmoja mmoja wakiendelea kutikisa na nyimbo zao. Ilikuwa ni Bumper to Bumper, ngoma kali.

Weusi walibaki kuwa weledi (professional), na hawakutumia ‘kiki’ au skendo zaidi ya kazi yao kuwa nzuri kila walipoamka na wimbo. Ni kundi la Hip Hop ambalo limekuwa likibadilika na kufanya nyimbo ‘laini’ kidogo. Wanajua soko linataka nini na wanajua kulitengenezea soko kitu cha kupenda.

Walifunga mwaka na NiCome.

 

Mtayarishaji Bora wa Muziki wa Kizazi Kipya – Laizer

Nyimbo nyingi zilizowapa tuzo kubwa wananii na hata kupiga hatua kubwa. Karibu nyimbo zote za WCB zimepikwa na mtayarishaji huyu na zimefanya makubwa kwa kipindi chote cha mwaka.

Laizer amefanya ngoma kubwa kama Halleluyah ya Diamond Platinumz na Morgan Heritage, Wakawaka ya Diamond na Rick Ross na zote kubwa kutoka kwa Bosi wake.

Hapa angechuana na watayarishaji wengine waliofanya nyimbo kubwa na bila shaka hii ni moja kati ya vipengele ambavyo vingezua gumzo kubwa. Wadau wangeweza kuuliza yuko wapi Harmy B ambaye mkono wake adhimu ulileta hits kama ‘Dume Suruali’, ‘Upo Hapo’ na nyingine? Yuko wapi Mr T-Touch mpishi wa hits nyingi za wakubwa na wadogo, wapi familia ya MJ Records n.k?

Huenda swali kubwa zaidi ni kwanini asiwe Man Walter aliyetengeneza Wimbo Bora wa Mwaka? Lakini jibu ni kwamba wimbo huo pekee usingetosha kupima hits zote za Laizer kwa mwaka jana.

 

Mtunzi Bora wa Nyimbo (Bongo Fleva)

Aslay

Aslay anastahili tuzo hii kwani mbali na kuachia nyimbo nyingi zaidi ya msanii yeyote kwa mwaka jana, nyimbo zote zilikuwa zinaonesha uwezo wake mkubwa wa utunzi wa mashairi na melodi. Shemeji, Natamba, Pusha, Acha Nilewe, Likizo na nyingine nyingi zitakupa sababu zaidi.

Hustler of The Year

Vanessa Mdee

Wengi wanahustle na heshima yao iko palepale, lakini kwa mwaka 2017, Msanii wa kike Vanessa Mdee anastahili tuzo hii bila upinzani mkali.

Ulikuwa mwaka mgumu sana kwake lakini aligeuza changamoto kuwa fursa.

Kwanza, akiwa katika hustle zake alihutuhumiwa kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya. Hata hivyo, baada ya kuachiwa kutoka selo za polisi, Vee hakuendelea kuomboleza, alitunga wimbo aliouita ‘Pumzi ya Mwisho’ unaopatikana kwenye albam yake inayotoka Januari mwaka huu ‘The Money Mondays’, akiwapa mashavu Cassper Nyovest na Joh Makini.

‘The Money Mondays’ yenye nyimbo rasmi 18 inaweza kuweka rekodi ya kuwa albam ya kisasa na bora zaidi kwenye kipimo cha kimataifa iliyowahi kutolewa na msanii wa kike nchini katika kipindi cha miaka 10 iliyopita. Tunafahamu kabla ya kutoka kwani tulishiriki kusikiliza nyimbo hizo mwishoni mwa wiki.

Alianzisha lebo yake ya muziki akiwasaini mdogo wake, Mimi Mars na wasanii wengine wapya kabisa. Baada ya kuhustle na kutengeneza albam nzito, amepata shavu la kuwa mwanafamilia ya Universal Music akipewa mkwanja mrefu kwa mujibu wake.

Walio karibu na Vee wanasema kuwa muda mwingi huzungumzia biashara na kutengeneza biashara zaidi.

Vee ameahidi kuachia albam yake nyingine akiwa chini ya Universal Music kabla ya kukamilika kwa nusu ya mwaka 2018.

Kabla ya mwaka kuisha, yeye na ndugu zake waliachia wimbo wa Injili ‘Beautiful Jesus’.

Man of The Year

Diamond Platinumz

Ulikuwa mwaka wa Diamod Platinumz kwa kila namna. Kwanza biashara ya karanga ambayo yeye ndiye brand na mwana hisa mkuu iliwapa ajira maelfu ya Watanzania nchini.

Pili, alipiga kolabo nzito ambazo hazijawahi kufanywa na msanii yoyote. Ni mwaka aliowashirikisha Rick Ross, Omarion, Neyo, Morgan Heritage, Mohombi na wengine wengi wakubwa kutoka Afrika.

Pia, alifanya matamasha mazito nchini, moja akiwa na Omarion na jingine akiwa na Future na Cassper Nyovest.

Bado Diamond aliendelea kuwa ‘Icon’ ya muziki wa Bongo Fleva nje ya mipaka ya Tanzania.

Msanii anayechipukia/ Kundi Jipya (Best New artist/Group

Mimi Mars & OMG

Mimi Mars ni msanii mpya aliyechipukia mwaka jana na kuweza kuingia kwenye orodha ya juu ya wasanii nchini. Akipewa nguvu na dada yake Vanessa Mdee aliingia kwenye muziki akiwa amekwiva na nyimbo zake Shuga, Dedee na Stamina zilifanya vizuri.

Mbali na Mimi Mars, huwezi kuacha kulitaja kundi la OMG lililo na wasanii bora. Kundi hili lililosikika kwa kishindo mwaka jana, linastahili tuzo hii. Nyimbo kama ‘Swing’, ‘Nikipata Gari’, ‘Uongo na Umbea’ feat. Baraka Da Prince unaweza kukupa sababu zaidi.

OMG na Boss wao Quick Rocka

Bonus

Shindano la Mwaka (Battle of Year)

Seduce Me Vs Zilipendwa

Hili ni shindano lisilo rasmi lililotia fora kwa mwaka 2017. Shindano hili liliasisiwa na uhasama wa wazi ulioibuka kati ya Boss wa WCB, Diamond Platinumz na Ali Kiba. Ni baada ya Diamond kumchapa bakora  ya maneno Ali Kiba kupitia freestyle yake juu ya mdundo wa wimbo wa Fid Q  ‘Fresh’. Kiba alijibu mashambulizi kupitia Twitter lakini alijibiwa tena kwa freestyle.

Wakati bado uhasama huo haujatulia, Ali Kiba aliachia ‘Seduce Me’ na siku iliyofuata WCB waliachia ‘Zilipendwa’. Ndipo mbio za shindano hilo zilipoanza, ni wimbo upi utapendwa zaidi.

Ni kama kila mwanafamilia wa Timu Kiba au Timu Diamond & wana- WCB alifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha timu yake inashinda.

WCB walijipanga kwa ‘All Out War’, yaani vita kamili kwa lugha ya kijeshi. Wasanii wote wakubwa wa kundi hilo walisikika kwenye ‘Zilipendwa’.

Gazeti moja kubwa liliandika habari iliyopambwa na kichwa ‘Diamond amuundia Alikiba Ukawa’.

Ni wazi kwamba ndani ya kipindi cha wiki mbili, ‘Seduce Me’ ilikuwa imeifunika ‘Zilipendwa’ YouTube na hata kwa kupiga kelele mitaani. Hata hivyo, nyimbo hizi mbili ziliteka anga na yeyote ambaye angeachia wimbo wake wakati huo angekuwa amefanya kosa la mwaka kwani hakuna ambaye angempa usikivu wa kutosha.

Hata hivyo, baada ya muda, Zilipendwa iliipita kwa mbali Seduce Me. Zilipendwa imemaliza mwaka ikiwa imetazamwa zaidi ya mara milioni 12 huku Seduce Me ikimaliza mwaka ikiwa imetazamwa zaidi ya mara milioni 8.

Unaweza kutoa maoni yako, tuanze kuumulika pia mwaka 2018.

Kisa cha raia wa kijerumani kuuawa kwa kisu Zanzibar
Joseph Mbilinyi aitwa kituo cha polisi

Comments

comments