Rapa Darasa amelazimika kujibebesha mzigo wa sakata la dereva anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida kwa kosa la kuhatarisha maisha ya abiria kwa kuachia usukani (staring wheel) huku akicheza wimbo wake mpya ‘Muziki’.

Kipande cha video kilichosambazwa WhatsApp kinamuonesha dereva huyo akicheza muziki huo kisha kuachia usukani na kuondoka kwenye kiti chake huku gari likiwa linaendelea kukimbia, kitendo kilichosababisha abiria wa pembeni yake kuwa anashikilia usukani kwa muda hadi dereva huyo aliporejea kwenye kiti chake.

Jeshi la Polisi mkoa wa Singida lilifanikiwa kumtia mbaroni dereva huyo katika eneo la Itigi na kuendelea na taratibu za kisheria dhidi yake baada ya kumhamishia Manyoni.

Akiongea na XXL ya Clouds Fm leo, Darasa amesema kuwa wanaendelea na jitihada za kuhakikisha dereva huyo pamoja na wenzake wanaachiwa ili waendelee na shughuli zao za kila siku kwani anaamini wamejifunza kutokana na makossa waliyoyafanya.

“Tuliambiwa wamehamishiwa kituo cha Manyoni. Kwahiyo mtu wetu pia tumemuelekeza aende Manyoni, akifika hapo ndio tutafahamu kinachoendelea ili tuweze kujua tunasaidiana nao vipi,” alisema Darassa.

Hata hivyo, rapa huyo amekiri kuwa kitendo alichokifanya dereva huyo sio cha kiungwana na kwamba kinahatarisha maisha, “walifikiria kitu kizuri kwenye mazingira mabaya.”

‘Muziki’, wimbo mpya wa Darassa akiwa amemshirikisha Ben Pol ni moja kati ya nyimbo kubwa zaidi za mwaka huu na hutosita kusema kwa sasa ndio wimbo namba moja wa rapa kutoka Tanzania unaosikilizwa kwa wingi mitaani na kupigwa redioni.

Makonda: Jitokezeni kwa wingi kwenye maadhimisho ya miaka 55 ya uhuru
Wazambia Kuipima Simba SC