Mlinda mlango mashuhuri wa Mashetani Wekundu David de Gea, ameisaini mkataba mpya ambao unamuwezesha kubaki Old Trafford, na kumaliza minon’gono ya kuondoka klabuni hapo.

De Gea alikua akihusishwa na taarifa za kuwa mbioni kuihama Manchester United kwa kipindi kirefu, kufuatia mkataba wake wa awali ambao ulitarajiwa kufikia kikomo mwishoni mwa msimu huu wa 2019/20.

Klabu nguli za barani Ulaya kama Real Madrid, Juventus na Paris Saint-Germain, ziliongoza kutajwa katika vita ya kuiwania saini yake mwishoni mwa msimu huu, lakini kwa sasa hazitokua na budi ya kuanza kutafuta njia mbadala ya kutimiza malengo yao.

Taarifa kutoka mjini Manchester zinaeleza kuwa, mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 28, amesaini mkataba wa miaka minne, ambao utafikia kikomo mwaka 2023.

Kwa mujibu wa mkataba mpya, De Gea atakua akilipwa mshahara wa Pauni 500,000 kwa juma, sawa na Alexis Sanchez ambaye alipelekwa kwa mkopo kwenye klabu ya Inter Milan ya Italia.

Mlinda mlango huyo kutoka nchini Hispania alijunga na Manchester United mwaka 2011, na mpaka sasa ameshaitumikia klabu hiyo katika michezo 367.

“Ni bahati na heshima kwangu kuendelea kuwepo hapa, tangu nimesajiliwa yapata miaka minane, nimeona hakuna haja ya kwenda mahala pengine zaidi ya kuendelea kuwa hapa,” alisema De Gea alipohojiwa na mwandishi wa habari wa tovuti ya klabu.

“Tangu nimeanza maisha hapa Manchester United, nimekua mwenye furaha, na siku zote ninashirikiana na wenzangu vizuri hadi kufikia hatua ya kucheza michezo zaidi ya 350, bado ninasema hii ni heshima kubwa sana kwangu.

“Nikiwa kama mchezaji ninapaswa kuvishwa taji na kuitwa mokongwe kwa muda niliokaa hapa, sina budi kuendelea kuwa sehemu ya timu na kuhakikisha ninashirikiana na kila mmoja, ili kufikia malengo ya kutwaa mataji.”

Kwa upande wa meneja wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer, naye amekiri kufurahishwa na hatua ya kukamilishwa kwa dili la mkataba mpya wa De Gea, huku akisema ilikua ndoto yake kumuona mlinda mlango huyo akiubaki katika himaya ya Old trafford.

“Ninaendelea kujivunia kuwa na mtu huyu, amekua muhimu sana tangu nilipoanza kazi hapa msimu uliopita kama meneja wa muda, nilijitahidi kadri nilivyoweza kumshawishi ili akubali kusiani makataba mpya, na leo yametimia, sina budi kujipongeza kwa kazi kubwa nilioifanya.” Alisema meneja huyo kutoka nchini Norway.

Manchestr United kwa sasa inashika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi ya England, na keshokutwa Alkhamis itakua mwenyeji wa Astana kwenye michuano ya Europa League, kabla ya kuwatembelea West Ham United mwishoni mwa juma hili, kwa ajili ya mpambano wa ligi ya PL.

Professor Jay afunguka agizo la Makonda, mahubiri kwenye kumbi za starehe
DED na DC waliokuwa na mgongano watumbuliwa