Aliyekua meneja wa klabu za Everton, Man Utd pamoja na Real Sociedad, David Moyes anatajwa kuwa sehemu ya wanaofikiriwa kukabidhiwa benchi la ufundi la klabu ya Aston Villa.

Moyes anafikiriwa katika nafasi hiyo ambayo pia inawaniwa na mameneja wengine wenye uzoefu na soka la nchini England kama Roberto Di Matteo pamoja na Nigel Pearson.

Inadaiwa kwamba, tayari Moyes ameshakutana na viongozi wa klabu ya Aston Villa ambayo kwa sasa ipo chini ya utawala wa kuibopa kutoka nchini China, Dr Tony Xia.

Hata hivyo inaelezwa kwamba, hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa na pande hizo mbili, hivyo suala la nani atakuwa meneja linabaki katika maamuzi ya uongozi wa Aston Villa.

Kuna uwezekano wa Roberto Di Matteo, kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho kufuatia mpango uliowekwa na viongozi wa klabu ya AS Roma ya nchini Italia, wa kutaka kumpa ajira huko Stadio Olympico, hivyo ushindani unatazamiwa kubaki kwa Moyes pamoja na Nigel Pearson.

Dr Tony Xia mwenye umri wa miaka 39, amedhamiria kuiona Aston Villa ikirejea kwenye mshike mshike wa ligi kuu, baada ya kushuka daraja msimu uliopita kwa kujenga utawala mpya wa klabu hiyo ili kufanikisha azma ya kuingia katika ushindani wa soka, akianza na ligi daraja la kwanza msimu ujao.

Wengine wanaotajwa katika safu ya uongozi mpya wa Aston Villa ni Christopher Samuelson, ambaye huenda akatangazwa kuwa mwenyekiti mtendaji, mfanyabiashara maarufu kutoka nchini Scotland Keith Wyness, anatazamiwa kuwa mtendaji mkuu.

Wyness, aliwahi kuwa mtendaji mkuu wa klabu za Aberdeen na Everton, zote za nchini England.

Adui Wa Liverpool Kujisogeza Nyumba Ya Jirani
Ryan Giggs Kuondoka Old Trafford