Gwiji wa klabu ya Arsenal David Andrew Seaman amemkingia kifua mlinda mlango Petr Cech na kushauri aachwe kikosini, ili asaidie kusaka mafanikio ya msimu wa 2018/19, licha ya kusajiliwa kwa mjerumani Bernd Leno.

Leno, amesajiliwa klabuni hapo katika kipindi hiki cha dirisha la usajili wa majira ya kiangazi akitokea Bayer Leverkusen, na tayari inaaminika huenda akawa chaguo la kwanza la meneja Unai Emery, huku fununu zikieleza kuna uwezekano wa Cech akauzwa kabla ya dirisha halijafungwa mwanzoni mwa mwezi ujao.

Seaman ambaye aliitumikia Arsenal kuanzia mwaka 1990–2003, amesmea kuna haja ya mlinda mlango huyo kutoka Jamuhuri ya Czech kubaki klabuni hapo, kutokana na uwezo na ujuzi alionao katika kipindi hiki ambacho Arsenal inahitaji kufikia lengo la kufanya vyema katika ligi na ikiwezekana kutwaa ubingwa.

Amesema suala la nani atakua chaguo la kwanza, halipi kipaumbele sana, lakini anaangalia umuhimu wa mlinda mlango huyo ambaye alisajiliwa na Arsenal mwaka 2015 akitokea Chelsea.

“Bado (Cech) ana uwezo mkubwa ambao unaweza kutoa changamoto kwa Leno, ambaye anahitaji kujifunza mengi kutoka kwake, binafsi sioni sababu ya kuanza kuhusishwa na taarifa za kuuzwa katika kipindi hiki, ninashauri abaki ili tuweze kuona ushindani wa kweli katika nafasi ya walinda mlango,” Alisema Seaman, ambaye alishinda mataji matatu ya ligi ya England akiwa na Arsenal.

“Ninakubaliana na sababu za umri ambazo mara nyingi zinatumika kama sababu za kuondolewa kwake kwenye kikosi cha kwanza, lakini tukumbuke umri kwa mlinda mlango sio tatizo, jambo kubwa ni kupewa nafasi kwa kushindanishwa na wengine, ndipo utaona uwezo na ujasiri alionao.”

Katika hatua nyingine Seaman akazungumzia uwepo wa mlinda mlango mwingine klabuni hapo David Ospina, ambaye anaendelea kutazamwa kama chaguo la pili.

Seaman amesema suala hilo halitowezekana kwa Ospina, kutokana na hitaji lake la kutaka kuthibitisha ana uwezo wa kuwa chaguo la kwanza, hivyo bado ushindani katika nafasi la kukaa langoni mwa Arsenal inaendelea kuwa na ushindani wa kweli.

“Sifikirii kama Ospina ataridhika na hatua ya kuendelea kuwa chaguo la pili, atafanya kila jitihada ili kuuthibitishia umma wa mashabiki wa Arsenal duniani kote kuwa, bado ana uwezo wa kupambana na kuwa chaguo la kwanza,” alisema Seaman.

“Haijalishi uwepo wa Leno ambaye ameletwa na meneja mpya, lakini binafsi naamini Ospina ana uwezo wa kupambania nafasi na kufanikiwa, hivyo kwa upande mwingine ushindani ninaouona huenda ukaleta ufanisi mkubwa katika lango la The Gunners msimu ujao.”

Klabu ya Arsenal, ilimaliza katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi ya England msimu uliopita, itaanza kampeni za kuwania ubingwa wa nchi hiyo msimu wa 2018/19 kwa kupambana na mabingwa watetezi Manchester City Agusti 12.

LIVE: Rais Magufuli akipokea Magawio kutoka Makampuni, Taasisi za Umma
LIVE: Rais Magufuli, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea wakishuhudia utiaji saini ujenzi wa Daraja la Salender