Kiungo mshambuliaji wa mabingwa wa soka nchini England Man City, David Silva, ametangaza kustaafu kuitumikia timu ya taifa ya Hispania, baada ya kuitumikia kwa muda wa miaka 12, huku akicheza michezo 125.

Silva mwenye umri wa miaka 32, alianza kuitumikia timu ya taifa ya Hispania mwaka 2006, na alikua sehemu ya kikosi kilichotwaa ubingwa wa dunia mwaka 2010, pamoja na ubingwa wa Ulaya mara mbili mfululizo 2008 na 2012.

Silva amethibitisha kustaafu kuitumikia timu ya taifa kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter kwa kuandika: ‘Ninashukuru kwa miaka yote niliyokua katika kikosi cha timu ya taifa ya Hispania, umewadia wakati wa kuondoka na kuwapisha wengine, ili waweze kutimiza jukumu la kuiwakilisha nchi yangu kwenye michuano ya kimataifa.’

Hatua ya kuthibitisha kuachana na timu ya taifa ya Hispania inamfanya ajiunge na wachezaji wengine ambao walitangulia kufanya hivyo kama Andres Iniesta na Gerard Pique, baada ya kikosi chao kuondolewa katika michuano ya kombe la dunia, hatua ya 16 bora kwa kufungwa na wenyeji Urusi kwa changamoto ya mikwaju ya penati.

“Sio rahisi kufikia maamuzi haya, lakini imenibidi baada ya kutoa mchango wangu katika timu ya taifa, nimejifunza mengi, na nimeshirikiana vizuri na wachezaaji wenzangu hadi kufikia mafanikio tuliyoyapata,” iliendelea kueleza taarifa iliyoandikwa na kiungo huyo kupitia Twitter.

Tangu alipoanza kuitumikia timu ya taifa ya Hispania mwaka 2006, Silva amefanikiwa kucheza michezo 125 na kufunga mabao 35.

TCU yatoa saa chache kufunga dirisha la maombi elimu ya juu
Video: kazi niliyotumwa ni hii, hayo ndiyo mambo natakiwa nifanye - Jerry Muro

Comments

comments