Wataalam wa tiba nchini Marekani kupitia Kampuni ya Merck, wametoa matumaini mapya kwa dunia baada ya kugundua dawa inayoweza kupambana na virusi vipya vya corona (covid-19) vilivyopewa jina la molnupiravir.

Kwa mujibu wa watalaam wa afya, molnupiravir ina uwezo wa kupunguza hatari ya kwa wagonjwa wa corona, ikipunguza kwa zaidi ya asilimia 50 uwezekano wa mgonjwa kufariki dunia au kulazwa hospitalini.

Taarifa za kupatikana kwa dawa hizo zilitolewa kwa mara ya kwanza Ijumaa baada ya kampuni hiyo kutoa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari kuhusu maendeleo ya dawa yake.

Molnupiravir, ambayo awali ilitengenezwa kwa lengo la kutibu mafua makali, imebainika kuwa na uwezo wa kuondoa changamoto ya covid-19. Dawa hizo ambazo zinatajwa kuwa na gharama nafuu ukilinganisha na dawa nyingine za kupunguza makali ya ugonjwa huo, dozi yake ni kidonge kimoja kutwa mara mbili kwa muda wa siku tano tu, kwa watu wazima.

Ikumbukwe kuwa hadi wakati huu, ni dawa aina ya remdesivir pekee nchini Marekani ambayo ilikuwa imepata kibali cha Mamlaka ya Chakula na Dawa ya nchi hiyo kama dawa wanayotumia wagonjwa wa corona, ambayo ilikuwa ikipitia moja kwa moja kwenye mfumo wa damu.

Kupitia utafiti walioufanya, kampuni hiyo ilitumia sampuli ya wagonjwa wa covid-19 watu wazima 775.

Utafiti huo uliofanyika kuanzia Agosti hadi Septemba 29 mwaka huu, ulibaini kuwa ni asilimia 7.3 tu ya wagonjwa waliotumia dawa ya molnupiravir waliopoteza maisha, na waliosalia walipona kikamilifu.

“Kwa matokeo haya, tunaamini kuwa molnupiravir inaweza kuwa dawa muhimu sana katika jitihada za dunia kupambana na janga la corona, na itaongeza heshima na upekee kwa kampuni yetu ya Merck,” alisema Afisa Mtendaji Mkuu wa Merck, Robert Davis.

Hata hivyo, Profesa Peter Hotez, mtaalam mbobezi wa tiba alisema kuwa ingawa dawa hizo ni hatua kubwa katika kupambana na covid-19, sio mbadala wa chanjo zinazoendelea kutolewa duniani kote.

Aliandika kupitia Twitter jumbe mbalimbali kuhusu dawa hiyo, akieleza kuwa sio tiba ya muujiza bali ni sawa na kifaa cha kuwapa faraja na tiba wagonjwa.

Hata hivyo, wataalam wanasubiri hatua za Shirika la Afya Duniani (WHO), kutoa kibali mahsusi baada ya kujiridhisha na tiba yoyote, ili dunia ifikiwe na tiba hiyo.

Kennedy ashonwa nyuzi sita
Habari kubwa kwenyemagazeti leo, Oktoba 5, 2021