Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri amepiga marufuku Askari wa usalama barabarani kusimamisha basi lolote njiani ndani ya wilaya yake baada ya kuondoka katika kituo kipya cha mabasi mjini Njombe badala yake wafanye ukaguzi kabla basi halijaanza safari.

Ameyasema hayo katika kikao cha wamiliki wa vyombo vya usafiri mkoa wa Njombe ambapo baadhi ya wamiliki wa vyombo vya usafiri wamelalamikia kukamatwa mara kwa mara na baadhi ya askari wa barabarani na kuwaweka kwenye vituo kwa muda mrefu hali inayopelekea kuwachelewesha abiria.

“Pale Stendi wamemruhusu na kama kuna mapungufu mmeona mmerekebisha na mmemruhusu sasa mnamsimamisha kituo kingine mara baada ya kutoka ndani kwa kosa lipi,anayekwenda ludewa akisha toka mle stendi ya mabasi hakuna kituo kingine chochote mpaka akiingia wilaya ya Ludewa huko ni kwingine, lakini ndani ya wilaya yangu mmeshamkagua mnataka mkague mara ngapi? Kama ameondoka amejaza watu hawezi kutoka utaratibu si upo,yaani si dakika tano, si mbili,si tatu hakuna kusimamisha aendelee na safari,”amesema Msafiri

Aidha, katika hatua nyingine wamiliki wa vyombo vya usafiri pia wamelalamikia kukosa ofisi za kukatia tiketi katika kituo kipya cha mabasi na uchache wa matundu ya vyoo katika kituo hicho ambacho kilianza kutoa huduma kabla ya kukamilika, kwa madai kuwa hali hiyo inawapa shida hasa kunapokuwa na mvua kwa kuwa wanakatia tiketi nje.

Kwa upande wake Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Njombe, Kubeja Ganja na Edwin Mwanzinga ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Njombe wakizungumzia kukosekana kwa vituo vya kushusha na kupakia abiria ndani ya mji wa Njombe wamesema kuwa uongozi wa halmashauri unaendelea kujipanga kuandaa vituo tofauti na ilivyo sasa ambapo hairuhusiwi mabasi kushusha au kupakia abiria nje ya kituo kipya cha mabasi mjini Njombe.

Video: JPM atoa agizo baada ya kupokea gawio kutoka TTCL
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Mei 22, 2019