Mkuu wa wilaya ya Nkasi, Saidi Mtanda amesema kuwa kama ikibainikika kuna mwananchi yeyote alipigwa na kuteswa wakati wa operesheni ya kuwaondoa wananchi waliovamia na kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya Msitu wa Hifadhi ya Mfili ambayo aliiongoza, atajiuzulu wadhifa huo.
Ameyasema hayo mjini Namanyere Nkasi mbele ya Naibu Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula alipokutana na watumishi wa Halmashauri ya Nkasi na kusikiliza kero za wananchi.
“Mimi mwenyewe ndio niliongoza operesheni hiyo na ninasema hakuna mwananchi yeyote aliyepigwa na kunyanyaswa na ninakiri kuna baadhi ya nyumba ziliteketezwa kwa moto, lakini kama kuna mtu yeyote aliyenyanyaswa na kuonewa niko teyari kujiuzulu mbele ya Naibu Waziri kwa sababu mimi ndio niliongoza zoezi hilo”alisema Mtanda.
Kwa upande wake mbunge wa wa jimbo la Nkasi kusini, Desderius Mipata amesema kuwa malalamiko ya wananchi ni ya kweli kwani Serikali wilani Nkasi ilitumia nguvu kubwa kuwatimua wananchi ndani ya msitu huo.
Hata hivyo Naibu Waziri Mabula, aliipongeza Serikali ya wilaya ya Nkasi kwa opresheni hiyo kwa kuzingatia sheria huku akiwashauri madiwani wafuate utratibu iwapo kama wanataka kubadilisha sheria ndogo ya mwaka 1998 inayoeleza kuwa msitu huo umehifadhiwa kisheria.