Na Allawi Kaboyo – Bukoba.

Mgogoro wa viwanja katika mtaa wa Kyebitembe Kata Nshambya Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera uliodumu kwa zaidi  ya miaka 22 na kusababisha kuwepo kwa viashiria vya uvunjifu wa amani sasa umemalizika baada ya serikali kuingilia kati..

Akiongea katika  mkutano wa hadhara na wananchi wa kata hiyo, Mkuu wa wilaya Bukoba Deodatus Kinawiro amesema kuwa  halmashauri ya Manispaa ya Bukoba kupitia kwa viongozi wake waliomaliza muda wao wakiongozwa na mstahiki Meya, walipanga kubomoa nyumba za wananchi 374 pamoja na misingi kwa kosa walilolifanya wao awali.

Kinawiro amesema serikali haipo tayari kuona wananchi wake wakiteseka na kuhangaika kwa makosa ya wataalamu waliokuwa wanahusika na masuala ya ardhi ambao walikuwa wakiuza kiwanja kimoja kwa zaidi  ya watu wawili na kusababisha migogoro.

“Mgogoro huu umedumu kwa miaka 22 na kuna watu wamekuwa wakinufaika na mgogoro huu bila kujali wananchi wanaoumia, sasa kuanzia sasa nafuta ramani ya zamani ili ichorwe ramani mpya ambayo itaendana na hali halisi ilivyo ya makazi ya sasa na kuanzia sasa pia hakuna kubomoa wala kugusa nyumba yoyote iliyojengwa hata msingi,” amesema Kinawiro.

Aidha ameiagiza halmashauri kuwatafutia viwanja ndani ya muda mfupi wale wote waliokuwa wakilalamikia viwanja ambavyo tayari viliuzwa na waliouziwa wameshajenga na wale waliokwisha jenga wasibughudhiwe.

Kwa upande wake Kaimu Kamishina wa Ardhi Mkoa wa Kagera Erick Makundi, amewataka wananchii kufuata utaratibu kabla  hawajanunua viwanja au kuanza ujenzi, na kuwa endapo watawahi kuchanga pesa za urasimishaji basi watapewa kipaumbele cha kupimiwa na suala la kupewa hati miliki halitazidi wiki mbili.

Mnamo Septemba 16, Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufui akiwa katika mkutano wa kampeni mjini Bukoba aliuagiza uongozi wa Wilaya ya Bukoba kuhakikisha wanamaliza mgogoro wa viwanja Kyebitembe mapema ili kuwawzesha wananchi kuishi kwa uhuru na usalama.

Wababe wa Israel wamsajili Novatus Dismas
Mourinho akoshwa na maamuzi yake