Aliyekuwa Miss Tanzania 2006, Wema Isaack Sepetu na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwagelo kila mmoja kwa wakati wake ametoa pongezi kubwa kwa mshindi wa shindano la Miss Tanzania 2018, Queen Elizabeth Makune na kupongeza jitihada zote zilizofanyika kufanikisha shindano hilo kwani limekuwa la haki na mlimbwende aliyepatikana kuiwakilisha Tanzania Duniani anastahili taji hilo kutokana na hali yake ya kujiamini.

Wema ameongezea kuwa amepanga kukutana na walimu pamoja na waandaji wa shindano hilo ili kushirikiana nao kumwandaa mrembo huyo kwa minajili ya kufanya vizuri katika shindano la mamiss wote duniani linalotarajiwa kufanyika Oktoba, 7 mwaka huu huko nchini Uphilipino.

“Kiukweli nimeridhishwa na mchakato wa upatikanaji wa Queen Elizabeth, alikuwa anastahili kushinda kutokana na hali ya kujiamini aliyokuwa nayo naamini kama tukimuandaa vizuri anaweza kwenda kufanya vizuri kwenye shindano la Dunia,” amesema Wema.

Aidha Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwagelo naye kupitia ukurasa wake wa instagram ametoa pongezi za dhati kwa Miss Tanzania 2018, Queen Elizabeth Makune kwa kushinda taji hilo na kumtakia baraka zote katika mashindano makubwa yajayo.

”Nenda ukapeperushe bendera ya Tanzania, una baraka zote kutoka kwetu. Kwa washiriki wote wa Miss Tanzania wa mwaka huu hongereni kwa kuweza kushiriki na kuyafanikisha mashindano haya na hiyo ni fursa pekee kwenu, muitumie kwa manufaa yenu pamoja na taifa“, ameandika Jokate.

Mhe. Jokate hakusita kutoa pongezi kwa mtayarishaji wa shindano hilo Basila Mwanukuzi kwa kuweza kurejesha heshima ya Miss Tanzania ambayo ilikuwa imepotea kwa miaka kadhaa kwa jamii pamoja na washiriki wenyewe.

Amesema “Kupitia wewe, wasichana watanufaika katika kutimiza ndoto zao kama neno linalovyosema ‘when something is important enough, you do it even if the odds are not in your favor’. Hongera sana dada yangu maana umefanikiwa kufanya ‘show’ kubwa hata bila ya kutegemea wadhamini na rasilimali za kutosha lakini hukukatishwa tamaa na hatimaye umeweza. ‘Looking forward to what the future holds for Miss Tanzania under your leadership and thank you for making that contribution for education in Kisarawe”, amesisitiza Jokate.

Nicki amuonya Cardi B, ‘utakufa’
Museveni azionya nchi za Magharibi na siasa yao, ‘kaeni mbali’