Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mkoani Mara, Charles Kabeho amewataka Mahakimu, Waendesha Mashtaka na Wanasheria  kutenda haki katika kesi zinazofikishwa mahakamani zikiwemo kesi za wananchi wanyonge ambao matumaini yao ni kuona Mahakama inawatendea haki.

Ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya Sheria yaliyofanyika katika Mahakama ya wilaya ya Tarime yaliyohudhuriwa na wadau mbalimbali baadhi yao wakiwemo watumishi wa Mahakama za Tarime.

Amesema kuwa haki ikitendeka inaleta imani kubwa kwa wananchi hasa wanyonge, lakini pia aliwataka wananchi kufika mahakamani kutoa ushahidi wa kweli kwani kwa kufanya hivyo itarahisisha kesi kukamilika haraka.

“Watendaji timizeni wajibu wenu kutatua mahitaji ya wananchi, wanyonge wapatiwe haki, mkitenda haki ni faraja kwa wananchi lakini pia niwaombe wananchi tutoe ushahidi wa kweli,”amesema Kabeho

Aidha, kwa upande wake hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Tarime, Veronica Mugendi ametaja baadhi ya changamoto zinazokwamisha haki kutendeka kwa wakati kuwa ni pamoja na wahusika kutofika kwa wakati mahakamani.

Naye Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Tarime, Lilian Gimunge amesema kuwa kuchelewa kwa upelelezi wa kesi inachangia ucheleweshaji wa kesi lakini pia amewataka watumishi kuwa waaminifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa huku akiwaomba wananchi kushirikiana kwa pamoja ili kusaidia kupunguza mlundikano wa kesi Mahakamani.

Hata hivyo, wakizungumza kwa nyakati tofauti na Dar24Media wakati wa maadhimisho hayo, Mwita Chacha Mkazi wa Mtaa wa Rebu kata yaTurwa amesema kuwa  baadhi ya wananchi wanaogopa kutoa ushahidi kutokana na kuhofia usalama wa maisha yao .

 

LIVE: Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akijibu Maswali ya Papo kwa Papo Bungeni Dodoma
Video: Tumepata Jaji Mkuu Mchapakazi- Prof. Lipumba