Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe Mkoani Njombe, Ally Kassinge ameagiza kwamba ukikutwa na mifuko ya plastiki katika wilaya hiyo ni kosa kisheria ni kama kukutwa na madawa ya kulevya aina ya bangi.

Ameyasema hayo katika Kata ya Ilembula wilayani humo wakati akizindua mifuko mbadala ambayo ni rafiki kwa mazingira ambapo Kassinge amewataka wananchi hao kusitisha matumizi ya mifuko hiyo ili kuepuka mkono wa sheria.

Ametoa wito kwa wajasiriamali wilayani humo kutumia fursa hiyo  kutengeneza mifuko mbadala kama mifuko ya karatasi na vikapu ambavyo ni rafiki wa mazingira.

‘’Nitumie nafasi hii kuwataka wajasiriamali wa wilaya yangu kutumia fursa ya kutengeneza mifuko ambayo ni rafiki wa mazingira ambayo itatosheleza mahitaji ya watu na hivyo mtakuza uchumi kwa familia au mtu mmoja mmoja,’’amesema Kassinge.

Kwa upande wake Mkurungenzi wa halmashauri ya wilaya ya wanging’ombe, Edes Lukoa amesema kuwa wananchi wapo tayari kutii sheria ya kutumia mifuko mbadala na kuachana na mifuko ya plastiki.

Naye afisa mazingira wa halmashauri ya wilaya ya wanging’ombe, Frank Ngogo amewataka wananchi kufuata sheria ili kuepuka adhabu endapo ataonekana na matumizi ya mifuko ya plastiki.

 

Wanafunzi kutoka nchini Ireland wapanda Miti mkoani Njombe
Watanzania 10,000 kupata ajira mradi wa bomba la mafuta ghafi