Mkuu wa Wilaya ya Njombe Mkoani humo, Ruth Msafiri ameshiriki katika hitimisho la ibada ya mfungo wa maombi ya kuuombea mkoa wa Njombe yaliyofanyika kwa wiki moja katika Kanisa la Tanzania Assemblies of God T.A.G lililopo mtaa wa Melinze halmashauri ya mji huo.

Akiwa katika ibada hiyo, DC Msafiri amewataka wakristo mkoani humo kuendelea kuombea mkoa wa Njombe kutokana na matatizo ya mauaji ya watoto yaliyojitokeza hivi karibuni huku akiwataka kuto kusahau kuombea masuala ya uchumi na familia kwa ujumla.

Amesema kuwa Serikali haijafurahishwa na mauaji hayo hivyo ni Wakati wa Kanisa Kuomba zaidi Ili Matendo hayo yapotee mkoani humo.

“Naendelea kuwategemea sana watu wa Mungu, hatutafika bila kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja, kama tumeagiza kwa lazima kila mzazi awe na mtoto kila wakati ni lazima uchumi utashuka, niwaambie kitu ambacho hamjajua halmashauri ya mji wa Njombe ni halmashauri ya kwanza Tanzania kwenye kipato cha juu kuliko halmashauri yeyote hapa nchini, mwananchi wa Njombe wa kawaida tu kipato chake hakipungui milioni tano kwa mwaka hii ipo Njombe mji tu kwa Tanzania,”amesema DC Msafiri

Kwa upande wake Mchungaji wa Kanisa hilo, Sefania Tweve amesema kuwa walikuwa na kazi kubwa ya kumlilia Mungu na kuombea mkoa wa Njombe, kuliombea Taifa, kuombea uchumi, kuombea ndoa pamoja na kushusha nguvu za giza kutokana na mambo maovu na ya kikatili yaliyotokea mkoani humo.

Hata hivyo, timu ya Wataalam kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) inayoongozwa na Hanifa Selengu imewasili mkoani Njombe kwa lengo la kuunganisha nguvu na Serikali ya Mkoa katika kupata namna bora ya kukomesha mauaji ya watoto yaliyotokea mkoani Njombe.

 

Guterres adai Afrika imeanza kukomaa Kidemokrasia
Video: Simulizi - Mtoto aliyekatwa koromeo, Nape - Sipingani na JPM,