Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida ameungana na Watanzania kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 17 ya kifo cha Baba wa Taifa na Rais wa Kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kufanya kongamano .
Katika Kongamano hilo lililofanyika Ikungi limejumuisha Viongozi wa kada tofauti wakiwemo viongozi wa serikali, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Vitongoji wa vijiji, Viongozi wa siasa, Wazee wa mji wa Ikungi, Maafisa Tarafa Watendaji, Madiwani, Walimu na wanafunzi ambapo wote kwa pamoja wamepata nafasi ya kuchangia mada na kupitisha maadhimio yatakayotoa taswira ya namna ya kumuenzi Mwalimu Nyerere.
Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu amewasihi wananchi kwa umoja wao kumuenzi Mwalimu Nyerere katika matendo makubwa na muhimu aliyokuwa anayafanya hususani misingi ya Haki, Ukweli na uwajibikaji.
Mtaturu amewataka watanzania kuishi katika misingi aliyoijenga Mwalimu Nyerere ikiwa ni pamoja na kutokubali kutoa na kupokea Rushwa kwani hayo ni miongoni mwa mambo aliyoyapiga vita wakati akiwa wa utawala wake.
Amesema kuwa Tanganyika wakati wa uhuru ilikuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo maradhi, ujinga na umasikini na kuongeza kuwa Mwalimu Nyerere alifanikiwa kupigana na maadui hao na kuimarisha upatikanaji mzuri wa huduma za afya na kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Kuendeleza Lugha ya Kiswahili, Kukuza Utu na uadilifu katika jamii.
Hata hivyo Mtaturu amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo hususani kusimamia vyema mapato ya serikali, Kupambana katika misingi ya utu, haki na usawa kwa kila raia , Kupinga rushwa na matumizi mabaya ya fedha za Umma
Kwaupande wake katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Ikungi Aluu Segamba amempongeza Mkuu huyo wa Wilaya kwa kuamua kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kufanya kongamano kwani imekuwa taswira njema kwa wakazi wa Wilaya hiyo ambao hawajawahi kushiriki katika kongamano kama hilo tangu kuanzishwa kwa Wilaya hiyo.
Kabla ya Kongamano hilo mkuu huyo wa Wilaya ya Ikungi akishirikiana na viongozi wote wa Wilaya pamoja na kamati ya ulinzi na usalama alitembelea Shule ya Msingi mchanganyiko Ikungi ili kutoa baadhi ya mahitaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu wakiwemo Wenye ulemavu wa ngozi, Walemavu mchanganyiko na wasioona.