Viongozi wa Vijiji  Wilayani Ikungi Mkoani Singida wameagizwa kusoma mapato na matumizi ili kuwarahisishia wananchi kufahamu jinsi fedha zao zinavyotumika kwa uwazi na kutoa fursa kwa wananchi kupata nafasi ya kuhoji ili kujiridhisha pale wanapokuwa na mashaka.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu wakati wa mikutano yake na  wakazi wa Wilaya hiyo iliyoanza jana kwa kutembelea kila kata kukagua miradi ya maendeleo na kufanya mikutano ya hadhara yenye lengo la kujua maeneo ya utendaji na kuwakumbusha wenyeviti na watendaji wa Vijiji na Kata kutambua majukumu yao.

Mtaturu ameagiza kufanyanyika uchunguzi ili kubaini kama kuna watendaji wamehamishwa kazi na wanatuhumiwa kuhujumu mapato ya serikali na michango ya wananchi kwa ajili ya shughuli za maendeleo kurudishwa haraka iwezekanavyo ili kutoa majibu ya tuhuma hizo na kuchukuliwa hatua endapo watabainika kujihusisha na kadhia hiyo.

Katika mkutano uliofanyika katika Kata ya Ntuntu na Kata ya Lighwa  Mtaturu amesema kuwa wazazi wote ambao watoto wao wanajihusisha na utoro mashuleni watachukuliwa hatua haraka iwezekanavyo ili kubaini chanzo cha utoro huo kama unasababishwa na wazazi wenyewe ama wanafunzi.

Hata hivyo Mtaturu amewakemea wanasiasa ambao wamezuia wananchi kuchangia ujenzi wa nyumba za walimu, Ujenzi wa Shule na maabara huku wakiwaahidi kuwa serikali itajenga kila kitu na kuongeza kuwa serikali kuu haiwezi kufanya kila jambo badala yake wananchi kwa umoja wao wanapaswa kushiriki katika uchangiaji wa huduma za kijamii.

Kwa upande wa wananchi waliohudhuria katika mkutano huo wamempongeza mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu kwa kufanya ziara katika Kata hizo kwani wana miaka zaidi ya 10 hawajawahi kutembelewa na Mkuu wa Wilaya wala Mkurugenzi

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu ameivunja kamati ya maji katika Kijiji cha Ntewa B iliyopewa mamlaka ya kuendeleza upatikanaji wa huduma ya maji na kumuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Bi Rustika Turuka kufatilia ili kujua chanzo cha kukosekana kwa maji katika kijiji hicho ilihali miundombinu ya kupatikana maji kijijini hapo imekamilika vyema.

TFF Yampa Jeuri Martin Saanya, Aibukia Mitandaoni
Waziri Mkuu atembelea gereza Isanga Dodoma