Benki ya Biashara ya DCB iliyopo chini ya, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), imetakiwa kuwajengea uwezo mzuri wateja wake katika kufanikisha mahitaji yao ya ujasiliamali ili kuweza kupata matokeo chanya na kupata kipato kizuri kitakacho wasaidia kuinua uchumi wa nchi.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Selemani Jafo alipotembelea Benki hiyo.

Jafo ameutaka uongozi wa Benki ya DCB kuwapatia elimu wateja wao juu ya kufanya ujasiliamali au biashara zao kwa kuwaongoza namna gani wataweza kufikia malengo yao katika shughuli wanazofanya ili kuhakikisha wanafikia malengo yao kwa ufasaha.

“Natoa wito kwenu kuwa mnatakiwa kuwa na ukarimu kwa wateja wenu ili kuweza kupata matokeo mazuri zaidi ya haya, kwani lugha nzuri utakayo tumia katika kumhudumia mteja wako ndo itakayo mfanya mteja kufurahia huduma yako na kupata wateja wengi zaidi ya hawa mlionao kwa sasa,”amesema Jafo.

Aidha, amesema kuwa sasa ni wakati wa DCB benki kujenga ushirikiano mzuri na uongozi wa jiji la Dodoma na wao kuwa na hisa katika benki hiyo kwani jiji la Dodoma ni miongoni mwa mikoa kumi inayofanya vyema katika ukusanyaji wa mapato hapa nchini .

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Biashara ya DCB, Godfrey Ndalahwa amesema kuwa mpaka sasa uboreshaji wa huduma na mahusiano ya wateja umekuwa ndio chachu ya kumuwezesha mteja kufungua akaunti na kufanya miamala yote ya kibenki, kutunza pesa na kuwekeza kwa kutumia simu yake ya mkononi.

Hata hivyo, Ndalahwa ameongezea kuwa benki ina malengo ya kujitanua zaidi tofauti na awali ilikuwa benki ya Jumuiya ya Wananchi wa Dar es salaam na kwasasa malengo ni kujitanua katika halmashauri, manispaa na majiji ya nchi nzima.

 

Nditiye akabidhi Kompyuta 25 Ludewa
Video: Familia yatoa ratiba rasmi mazishi ya Ruge Mutahaba

Comments

comments