Uongozi wa klabu ya Manchester United una matumaini ya kufikia makubaliano na mlinda mlango David de Gea, ya kusaini mkataba mpya ambao utamuweka Old Trafford kwa kipindi kirefu.

De Gea mwenye umri wa miaka 27, anapigiwa upatu wa kusaini mkataba mpya klabuni hapo, kufuatia mkataba wa sasa kutarajia kufikia kikomo mwaka 2019, huku hofu ikitanda miongoni mwa viongozi wa Man Utd kwa kuamini huenda mlinda mlango huyo akatumia nafasi hiyo kuondoka.

Awali ilikua inahofiwa huenda De Gea angetimkia Real Madrid, lakini kusajiliwa kwa Thibaut Courtois juma lililopita akitokea Chelsea kwa kiasi cha Pauni milioni 35, kumeondoa fikra za mtu huyo kuondoka na kurejea nyumbani kwao Hispania.

Real Madrid walikua wanahusishwa na mpango wa kutaka kumsajili De Gea tangu mwaka 2015, lakini walishindwa kutokana na mipango na mikakati madhubuti iliyowekwa na viongozi wa Man Utd kwa kipindi hicho.

Hata hivyo bado kuna wasi wasi wa mabingwa hao wa Ulaya wakarejea tena kwa De Gea, endapo shughuli ya kusainiwa mkataba mpya haitofanikiwa, na hii itatokana na kiwango cha Thibaut Courtois, kama kitaridhisha kwa msimu huu wa 2018/19.

Mazungumzo baina ya pande hizo mbili yanaendelea kwa sasa, lakini bado mlinda mlango De Gea amekua akisisitiza baadhi ya mambo katika mktaba huo mpya, ambayo yameegemea sana kwenye maslahi yake binafsi.

Mwezi Mei mwaka huu, De Gea ambaye alijiunga na klabu ya Man Utd akitokea Atletico Madrid mwaka 2011 kwa ada ya Pauni milioni 18.9, alitangazwa kuwa mchezaji bora wa klabu kwa msimu wa 2017/18, ikiwa ni mara yake ya nne mfululizo.

Pia alitajwa kuwa kwenye kikosi bora cha chama cha wachezaji wa kulipwa nchini England (PFA) kwa msimu wa 2017/18.

Akiwa na timu ya taifa ya Hispania wakati wa fainali za kombe la dunia nchini Urusi, De Gea  hakuonyesha kiwango cha kuridhishwa, huku akifanya makosa katika mchezo wa kwanza hatua ya makundi na kusababisha kufungwa kizembe na mshambuliaji wa Ureno, Cristiano Ronaldo.

Msimu huu wa 2018/19 tayari ameshaitumikia klabu yake katika mchezo mmoja dhidi ya Leicester City, na amekubali kufungwa bao moja, huku Man Utd wakichomoza na ushindi wa mabao mawili.

Wabunge mbaroni kwa kushambulia gari la Rais
Video: Zitto avaana na Nape..., Chadema yaja na uamuzi mgumu

Comments

comments