Hatimae kiungo mshambuliaji kutoka nchini England Dele Alli, amekubali kusaini mkataba wa muda mrefu na klabu ya Tottenham Hotspur, ambao utamuwezesha kufanya kazi kaskazini mwa jijini London hadi mwaka 2024.

Taarifa zilizotolewa na uongozi wa Tottenham Hotspur zimeeleza kuwa, Alli ameafiki kusiani mkataba huo, baada ya mazungumzo ya muda mrefu na uongozi.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 22, ambaye alisajiliwa na Spurs akitokea Milton Keynes Dons mwaka 2015, amekua muhimili mkubwa kwenye kikosi cha Mauricio Pochettino, na msimu uliopita alitangazwa kuwa mchezaji bora mwenye umri mdogo kupitia chama cha wachezaji wa soka nchini England (PFA), sambamba na kuwa miongoni mwa wachezaji waliounda kikosi bora cha ligi ya England.

Mpaka leo anakubali kusaini mkataba wa miaka sita, Alli ameshaifungia Spurs mabao 48 katika michezo 153 aliyocheza.

Alli pia amekua mchezaji muhimu kwenye kikosi cha timu ya taifa ya England, chini ya kocha mzawa Gareth Southgate, na tayari ameitumikia timu hiyo mara 31 tangu mwaka 2015.

Spurs inaendelea kufanikiwa katika ushawishi wa kuwasainisha mikataba mipya wachezaji wake, baada ya kufanya hivyo mwanzoni mwa mwaka huu kwa mshambuliaji Harry Kane, beki Davinson Sanchez na washambuliaji wa pembeni Erik Lamela na Son Heung-min.

Meneja wa kikosi cha Spurs Pochettino, naye alikubali kusaini mkataba mpya wa kuendelea kufanya kazi na klabu hiyo mwezi Mei mwaka huu, ambao utafikia kikomo mwaka 2023.

Ray C amshika mkono Wema, "Bado nina imani na wewe"
FC Barcelona yapanga kumuuza Ousmane Dembele