Mshambulaiji kutoka nchini Senegal na klabu ya Shanghai Shenhua Demba Ba, amemaliza utata kuhusu mustakabali wa soka lake baada ya kuvunjika mguu akiwa katika mchezo wa ligi kuu ya soka nchini China mwishoni mwa juma lililopita.

Ba, amemaliza utata huo baada ya kuthibitisha ataendelea kucheza soka atakapopona majeraha ya mguu wake wa kushoto ambao ulivunjika vibaya baada ya kuchezewa rafu na beki wa Sun Xiang alipokua katika harakati za kulishambulia lango la Shanghai SIPG.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 31, ametoa uhakika huo akiwa hospitali akiendelea na matibabu, ambapo aliwaambia waandishi wa habari waliomtembelea kwamba, hafikirii kuachana na soka.

“Kweli ni jeraha baya, lakini ninaamini nitarejea uwanjani na kucheza soka kama kawaida,” Alisema Ba

Utata wa kustaafu kwa Ba, uliibuka baada ya kocha wa kikosi cha Shanghai Shenhua, Gregorio Manzano kuonyesha wasiwasi wa kumkosa mshambuliaji huyo mara baada ya kuumia ambapo alijikuta akisema mbele ya vyombo vya habari “Huenda akastaafu soka”.

Ba, alijiunga na klabu ya Shanghai Shenhua akitokea nchini Uturuki alipokua akiitumikia klabu ya Besiktas ambayo ilikubali kumuuza kwa kiasi cha Pauni milioni 12 mwezi Julai mwaka 2015, na kwa sasa ndiye anaeongoza kwa upachikaji wa mabao katika ligi ya nchini China kwa kufunga mabao 14, katika michezo 18 aliyocheza.

Video: Kiwanda cha Pepsi Kulipa Faini ya Milioni 25 Kwa Uchafuzi wa Mazingira
Mashabiki Wa Arsenal Wapingana Na Babu Wenger