Kwa ushawishi mkubwa wa Kocha wa Ihefu FC Zubeir Katwila, hatimaye uongozi wa klabu hiyo ya mkoani Mbeya umefanikisha lengo la kumsajili  mlinda mlango Deogratius Munish ‘Dida’ kama mchezaji huru katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili, ambacho kilianza rasmi juzi Jumatano (Desemba 16).

Kwa majuma kadhaa Ihefu FC ilikua inahusishwa na mpango wa kumsajili mlinda mlango huyo, ambaye aliwahi kuzitumikia klabu nguli nchini Tanzania Simba SC, Young Africans na Azam FC, na wamedhihirisha hilo leo Ijumaa (Desemba 16) kwa kuanika picha zake mitandaoni akisaini mkataba akiwa na jezi za klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya kwanza msimu huu 2020/21.

Akizungjmza baada ya kufanikisha usajili mlinda mlango huyo ambaye aliwahi kuwa chaguo la kwanza kwenye timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Kocha Katwila amesema lengo la kusajili wachezaji wenye uzoefu na Ligi Kuu Bara ni kuongeza hali ya kujiamini na kupambana kwa vijana wake kwenye mechi zote zilizobaki.

“Ninahitaji kuwa na wachezjai wenye uzoefu kama ‘Dida’, ninaamini katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili tutawapata wawili watatu, watatusaidia kufanikisha lengo la kupambana kwenye michezo yetu ya Ligi Kuu.” Amesema Katwila.

Msimu uliopita Dida alisajiliwa Lipuli FC, ambayo ilishuka daraja kutoka Ligi Kuu hadi Ligi Daraja la Kwanza.

Busquets aingia anga za Messi FC Barcelona
Wawili kuongezwa Young Africans