Kipigo kilichoishtua dunia ya masumbwi usiku wa kuamkia leo alichoshushiwa bondia Muingereza, Anthony Joshua (AJ) katika pambano lake la kwanza nchini Marekani dhidi ya Mmexico, Andy Ruiz aka Destroyer kimemuibua hasimu wake, Deontay Wilder.

AJ ambaye aliingia kwenye pambano hilo jana usiku akijiamini na kupewa asilimia kubwa zaidi ya kuwa mshindi, alichakazwa kwa kipigo cha KO, akiangushwa mara mbili katika raundi ya tatu na raundi ya saba akaangushwa kwa masumbwi mazito yaliyomfanya amuombe mwamuzi amalize pambano.

Mbali na kipigo cha KO, Ruiz ambaye wengi walikuwa wanamtania kuwa ni ‘kibonge nyanya’ alimzidi kwa mbali AJ na kumiliki pambano.

Kutokana na matokeo hayo, Deontay ambaye siku zote amekuwa akidai AJ hawezi kusimama naye ulingoni, ameandika kwenye Instagram akidai kuwa bondia huyo hajawahi kuwa bingwa wa kweli wa dunia bali amekuwa akibebwa na kupewa ushindi kama zawadi.

“Hakuwa bingwa wa kweli. Maisha yake yote ya ubondia ulijaa uongo, utata na zawadi. Ukweli, na sasa tunajua alikuwa anamkimbia nani #hadileo,” tafsiri isiyo rasmi ya ujumbe wa Wilder.

Awali kumekuwa na maneno mengi kuhusu kutofanyika kwa pambano kati yao, kila mmoja akimrushia lawama mwenzake kuwa ndiye kikwazo.

Baada ya matokeo ya leo, AJ ambaye alikuwa hajawahi kupigwa katika mapambano yake 22, alimpa heshima Ruiz na kuwaomba radhi mashabiki wake kwa kuwaangusha. Ruiz amewahi kupoteza pambano moja tu kati ya mapambano yake 35 sasa.

AJ na Ruiz wanapaswa kuwa na pambano la marudiano kwa mujibu wa mkataba wao.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Juni 3, 2019
Mgalu: Kila Kijiji kitapata Umeme

Comments

comments