Bingwa wa dunia wa masumbwi ya uzito wa juu, Deontay Wilder amesema kuwa anajisikia kama amegeuka kuwa muuaji kabla ya pambano lake na mbabe kutoka Uingereza, Tyson Fury.

Wilder na Fury watapanda ulingoni kuoneshana ubabe Disemba Mosi mwaka huu, Los Angeles Marekani, katika pambano ambalo linatajwa kuwa pambano la uzito wa juu litakaloingiza fedha nyingi zaidi kwa mwaka huu nchini humo.

Wilder ambaye hajawahi kushindwa katika mapambano yake 40, amesema, “najisikia mwili wangu umebadilika kabisa, niko tayari kwa mauaji.”

Hata hivyo, Wilder alisema kuwa hatamzungumzia mbabe Anthony Joshua kwa madai kuwa alimuogopa na kwamba akili na macho yake sasa hivi ni kwa Fury.

“Sitaki mtu yeyote aniulize kuhusu Anthony Joshua. Alikuwa muoga na hivyo ndivyo ilivyo. Sina ujumbe wowote kwake, sasa hivi ni Tyson Fury. Najisikia kama muuaji, nimebadilika kuwa muuaji,” alisema.

Hata hivyo, mapema mwezi Juni, Joshua alisema kuwa anaamini uwanja wa Wembley ambao umeshalipiwa kwa ajili ya pambano lake Aprili 13 mwakani, utashuhudia pambano kati yake na Wilder.

Kwa upande mwingine, wakati Wilder anadai kujisikia kumuua Fury, mbabe huyo wa Uingereza amesema kuwa atabadili upepo kwa kumpiga kwa KO kisha achukue nafasi ya kupigana na Joshua.

Raila atangaza kung’atuka siasa za kuwania urais 2022
Ali Kiba ajibu mualiko wa Diamond Wasafi Festival, ‘kisanii’

Comments

comments