Uongozi wa shirikisho la soka nchini Ujerumani DFB umekanusha kuwepo kwa tuhuma  za ubaguzi wa rangi dhidi ya kiungo mshambuliaji wa klabu ya Arsenal Mesut Ozil, ambaye aliotoa madai ya kuwepo kwa tatizo hilo baada ya kushambuliwa na mashabiki kupitia mitandao ya kijamii.

Ozil, mwenye umri wa miaka 29, alitangaza kujiuzulu kuitumikia timu ya taifa ya Ujerumani mwishoni mwa juma lililopita, kwa kutaja sababu ya ubaguzi wa rangi na ukosefu wa heshima kuwa chanzo cha kutangaza maamuzi hayo.

Mchezaji huyo amesema alipokea barua za chuki na vitisho na alilaumiwa baada ya timu ya taifa ya Ujerumani kuondolewa kwenye fainali za kombe la dunia zilizofanyika nchini Urusi.

Taarifa iliyotolewa na shirikisho la soka nchini Ujerumani imeeleza: “Hatukubaliani na madai yaliyotolewa na Ozil kuhusu kuwepo kwa ubaguzi wa rangi. DFB tumepambana kwa kipindi kirefu katika hatua za kuijenga timu yetu na tulihakikisha suala hilo halipewi nafasi hata siku moja.”

Ozil alishutumiwa na mashabiki wa soka kupitia vyombo vya habari vya Ujerumani baada ya kupigwa picha na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan mwezi Mei katika hafla iliyofanyika jijini London.

Mbali na mashabiki wa soka, pia wanasiasa wa Ujerumani waliwakosoa Ozil na Gundogan na kuwatilia shaka kuhusu uzalendo wa nchi yao.

Hata hivyo wachezaji hao walikutana na rais wa shirikisho la soka Ujerumani kuelezea kilichotokea, licha ya kwamba Ozil hakutoa tamko hilo hadharani kuhusu suala hilo hadi juzi Jumapili.

Ujerumani awali ilikuwa imemkosoa rais huyo wa Uturuki kutokana na kampeni zake dhidi ya wapinzani kufuatia mapinduzi yaliyoshindikana nchini humo.

Katika hafla iliyofanyika jijini London Rais Erdogan alikutana na Malkia wa Uingereza na waziri mkuu Theresa May, na Ozil alieleza kwamba angekuwa amewakosea heshima mababu zake iwapo angekataa kupigwa picha na rais wa Uturuki.

Ozil, ambaye kizazi chake cha tatu ni Mjerumani mwenye asili ya Uturuki, alizaliwa huko Gelsenkirchen na alikuwa miongoni mwa wachezaji waliofanikisha azma ya kutwaa taji la dunia mwaka 2014, nchini Brazil.

Mwezi mmoja kabla ya Ujerumani kutetea taji lake, Ozil alikutana na rais wa Uturuki Erdogan pamoja na Ilkay Gundogan anaeitumikia klabu ya Manchester City ambaye pia ana asili ya Uturuki.

Baadae picha zilisambazwa na chama tawala cha Uturuki AK Party kuelekea uchaguzi mkuu wa nchi hiyo ambapo Erdogan aliibuka mshindi mwezi uliopita.

Lugola amsweka ndani askari polisi kwa uzembe
DataVision International, DC Mjema kuja na mradi wa kuwasaidia madereva Bodaboda na Bajaji