Dhahabu ya Bilioni 34.3 imeuzwa katika Kipindi cha mwezi mmoja kupitia katika masoko 21 yaliyoanzishwa kwa ajili ya kuuza madini katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

Hayo yamesemwa Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Madini, Dotto Biteko ambapo amesema kuwa kuanzishwa kwa masoko hayo kumekuwa chachu ya kuongeza mchango wa sekta ya madini katika kukuza uchumi na pato la Taifa kwa ujumla.

“Katika kipindi cha mwezi mmoja tu yaani Machi 17 mpaka Aprili 17 mwaka huu, jumla ya kilo 409.3 za dhahabu pekee zenye thamani ya shiilingi bilioni 34.3 imeuzwa kupitia katika maduka yaliyoanzishwa katika mikoa mbalimbali, katika kilo hizo,Mkoa wa Geita umeongoza kwa kufanya biashara ya jumla ya kilo 289, Kahama kilo 44, Mara kilo 13, lakini cha kufurahisha zaidi ni kwa Wilaya ya Chunya ambako jumla ya kilo 52 zimeuzwa katika soko hilo zikiwa ni siku chache toka kufunguliwa kwake,”amesema Biteko.

Amesema kuwa kuridhishwa na biashara inayofanyika katika maduka hayo ya madini kote nchini na kueleza kuwa licha ya mafanikio hayo yaliyofikiwa katika kipindi kifupi,serikali inashughulikia changamoto ndogo ndogo ikiwemo wafanyakazi, mashine za XRF na idadi ya watoa vibali.

Aidha, amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuona sekta hiyo inatoa mchango stahiki katika kujenga uchumi na kuchangia maendeleo hapa nchini ndio sababu mkazo umewekwa katika kusimamia sekta hii.

Hata hivyo, amewataka wachimbaji wadogo wadogo na madalali wa madini kuhakikisha kuwa wanatumia masoko hayo kikamilifu na kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufutiwa leseni jambo alilosema serikali haipendi,

Baadhi ya Mikoa ambayo imeshafungua masoko ya kuuza madini ni pamoja na Geita, Dodoma, Mwanza, Tabora, Shinyanga, Morogoro, Mbeya, ambapo tayari mikoa 21 imeshafungua maduka hayo hadi sasa ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli alilolitoa kwa wakuu wa mikoa wote hapa nchini.

Samatta atua Tanzania, aahidi makubwa AFCON
Nchi 21 zashiriki Uchaguzi wa bunge la Ulaya