Mshambuliaji, Elias Maguli  amekamilisha usajili wa kujiunga na klabu ya klabu ya Dhofar SC, inayoshiriki ligi kuu ya soka nchini Oman (Oman Professional League).

Maguli amejiunga na klabu hiyo iliyomaliza katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi ya nchini Oman, kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake wa mwaka mmoja na klabu ya Stand Utd ya mkoani Shinyanga.

Maguli ameondoka nchini akiwa amefunga jumla ya magoli 33 katika misimu yake mitatu aliyocheza kama mchezaji wa klabu za Ruvu Shooting, Simba na Stand United.

Ameruka vikwazo vingi katika soka la Tanzania ambalo limezunguukwa na kila aina ya figisu figisu na matatizo mengi ya watendaji. Mfano, katika misimu yake miwili ya mwisho VPL (Simba na Stand) timu hizo zote mbili zimejaa migogoro ya kiutendaji kati ya viongozi na wachezaji au viongozi kwa viongozi.

Katika mazingira hayo si rahisi kwa mchezaji kutimiza malengo yake na inapotokea nafasi kama hii ya Maguli-Kusajiliwa moja kwa moja na timu ya kulipwa ukiwa U25 ni jambo la kumshukuru Mungu na pengine ni sehemu ya kufanya kazi nzuri zaidi kwa jitihada ili kuthibitisha kwa wale waliokusaini kuwa hawakufanya makosa.

Maguli ni mshambuliaji wa kikosi cha kwanza katika timu ya Taifa ya Tanzania kwa mwaka mmoja sasa akicheza sambamba na Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta katika safu ya mashambulizi kwa maana hiyo, kocha Charles Mkwassa ataendelea kufurahia vijana wake watatu wakiwa ng’ambo ya nchi kuendeleza vipaji vyao na kudumisha viwango vyao vya kiuchezaji.

Kama Hamis Mroki anayecheza Thailand, huyu ni nahodha wa kikosi cha vijana kilichokuwa kikiwajumuhisha kina Ulimwengu, Himid Mao na wengine ni zao la TSA, Samatta, Tom, Maguli, Mrisho Ngassa watatupiwa jicho la 3 bila shaka timu ya Taifa Stars itaimarika licha ya kwamba bado hatuna ligi makini ya ndani.

Dhofar ni timu iliyoanzishwa miaka 44 iliyopita, na Oman kuna mishahara mikubwa hadi kufikia dola 30,000 kwa mchezaji wa kiwango cha Maguli. Mchezaji wa kikosi cha kwanza wa timu ya Taifa. Sasa mastaa watatu wa Stars katika kikosi cha mashambulizi wapo ng’ambo. Kila la heri Elius Maguli.

Wabunge wa Ukawa waja kivingine, ni nyeusi tupu na mabango
Wanawake Zaidi Kufanya Maamuzi ya Kura katika Tuzo za Oscar