Bosi wa WCB, Diamond Platinumz ameeleza jinsi ambavyo amepanga kuuteka ulimwengu wa burudani baada ya kushinda tuzo kadhaa na kuwa miongoni mwa ‘Orodha A’ ya wasanii wa Afrika.

Diamond amesema kuwa albam yake ya ‘A Boy From Tandale’ anaichukulia kama albam yake ya kwanza ingawa amewahi kutoa albam kadhaa kwa sababu imebeba lengo kubwa la kuiweka kiganjani dunia ya muziki.

Akiongea na BBC hivi karibuni, Chibu amesema kuwa ndani ya albam hiyo amewashirikisha wasanii wakubwa duniani ambao watasaidia pia kuisukuma Bongo Fleva kupanda kwenye kilele cha muziki pendwa duniani.

“Naiona kama albam yangu ya kwanza. Ndio maana unaona nimewashirikisha wasanii kama Rick Ross, Neyo, Omarion na wengine ambao siwezi kuwataja sasa hivi,” Diamond amefunguka.

 

Amesema wimbo wake na Rick Ross ambao unaitwa ‘Waka’ amechanganya Kiswahili na kiingereza kama alivyofanya kwenye kolabo nyingine.

Mbali na wasanii wa nje, amesema amewapa shavu pia wasanii wa ndani akiwemo rapa Young Killer.

Kuhusu mauzo ya albam hiyo, amesema atatumia njia za mauzo zinazotumiwa na wanamuziki wengine wakubwa kupitia mitandao husika inayofanya mauzo kimataifa.

Diamond ameenda nchini Uingereza kufanya ziara ya vyombo vya habari lakini atarejea huko mwezi ujao kwa ajili ya kufanya ‘show.

Video: Vita mpya yaibuka kati ya Nyalandu na Kigwangalla, Zito njia panda...
Magazeti ya Tanzania leo Novemba 14, 2017