Diamond Platinumz amevunja ukimya kuhusu tuhuma dhidi yake zilizotolewa na Ali Kiba siku chache zilizopita, tuhuma zilizozua gumzo zaidi kupitia mfano wa kumuibia penseli kisha kumsaidia aliyeibiwa kuitafuta.

Mashambulizi ya Ali Kiba yalikuja saa chache baada ya Diamond kueleza kuwa yeye na uongozi wa WCB wanafanya mawasiliano na uongozi wa Ali Kiba ili naye aweze kupanda kwenye jukwaa la Wasafi Festival.

King Kiba aliandika, “Usiniletee mambo ya darasa la Pili unaniiibia penseli alafu unanisaidia kutafuta (UNIKOME).  Mwanaume huwa anaongeaga mara moja tu sasa ukitaka nikuweke uchi watu wajue unayonifanyia hata kwenye hilo tamasha hatokuja mtu sasa tuishie hapo nakutakia tamasha njema @diamondplatnumz.

Jana, Diamond alifunguka kupitia kipindi cha Block 89 cha Wasafi FM, alipoulizwa kuhusu ujumbe wa Ali Kiba dhidi yake.

“Mimi pia nilifanikiwa kuona kama watu wengine walivyoona. Lakini unajua Ali ni kaka yangu. Amenizidi umri, alianza muziki kabla yangu mimi. Kwenye mambo ya muziki unajua tena unapotoa wimbo inakuwa kama mambo ya u-Simba na Yanga,” alisema.

“Lakini haiwezi kuwa inaweka chuki katika moyo wangu mimi, na haiwezi kuweka chuki katika moyo wake yeye. Ingawa sijajua aliandika vile kwa sababu gani, lakini ni mtu ambaye mimi ninamheshimu sana. Na mimi na yeye ni watu ambao tunachangia kuliletea heshima taifa letu kupitia muziki,” aliongeza.

Alipoulizwa kwanini hakujibu, alisema hakuwa na jibu lolote.

Katika hatua nyingine, Diamond na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakiwa katika kipindi hicho walifanikiwa kuchangisha Sh. 80 Milioni ambazo zitafanikisha matibabu ya moyo kwa watoto 40 kati ya watoto wengi wanaohitaji huduma hiyo. Zoezi la kuchangia linaendelea.

IGP Sirro aagiza aliyetishia bastola ajisalimishe polisi, mitandao yamtaja
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Novemba 2, 2019