Mlinda Lango wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Djigui Diara huenda akaukosa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2022/23, dhidi Polisi Tanzania utakaopigwa leo Jumanne (Agosti 16).

Miamba hiyo itakutana Uso kwa Macho katika Uwanja wa Sheikh Ameri Abeid, baada ya Maafande wa Jeshi la Polisi kuhamishia makazi yao mjini Arusha, kufuatia Uwanja wao wa Ushirika Moshi kufungiwa na TFF kwa kigezo cha kukosa sifa za kutumika katika michuano ya Ligi Kuu.

Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi amesema Diara anasumbuliwa na maumivu aliyoyapata kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, baada ya kugongana na Kiungo Mshambuliaji wa Simba SC Pape Sakho.

Amesema kucheza ama kutokucheza mchezo dhidi ya Polisi Tanzania kutategemea na hali ya Malinda Lango huyo itakavyokuwa, huku akitegemea ushauri kutoka kwa timu ya Madaktari.

“Tuna majeruhi wachache ambao tutahitaji kuangalia maendeleo yao katika mazoezi yetu kule Arusha, Lomalisa Joyce alikuwa na maumivu kidogo, Diarra Djigui aligongana na Pape Sakho kwenye mechi iliyopita tunahitaji kujiridhisha kama watakuwa tayari kwa mechi hii dhidi ya Polisi.”

Kuhusu mchezo wa leo, Kocha huyo kutoka nchini Tunisia amesema amewahimiza Wachezaji wake kupambana kama ilivyokua msimu uliopita, pia amewasihi kusahau furaha ya ushindi walioupata dhidi ya Simba SC Jumamosi (Agosti 13).

“Nimemwambia wachezaji wangu kwamba wasahau furaha ya ushindi dhidi ya Simba, hiyo ni mechi ambayo imeshapita sasa kila mmoja wetu akili yake iwe dhidi ya Polisi.”

“Polisi ni timu ngumu kila tunapokutana haujawahi kuwa mchezo rahisi, Young Africans tumejiandaa tunahitaji kuanza kwa nguvu ligi katika kuweza kuweka hai malengo yetu.” amesema Kocha Nabi
Msimu wa Ligi Kuu 2022/23 ulianza rasmi jana Jumatatu (Agosti 15) kwa michezo miwili kuchezwa katika viwanja na majira tofauti.

Ihefu FC waliikaribisha Ruvu Shooting katika Uwanja wa Highland Estate Mjini Mbarali mkoani Mbeya majira ya saa 10:00 jioni huku Namungo nao waliwaalika Mtibwa Sugar kutoka mkoani Morogoro Majira ya saa 1:00 usiku Uwanja wa Benjamini Mkapa.

Ihefu FC iliyorejea Ligi Kuu ikitokea Ligi Daraja la Kwanza, ilianza vibaya michuano hiyo baada ya kukubali kufungwa 1-0 na wageni wao Ruvu Shooting kutoka Mlandizi mkoani Pwani.

Kwa Upande wa Namungo FC mambo yaliwaendea Kombo baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 wakiwa nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambao wanautumia katika kipindi hiki kufuatia Uwanja wao wa Majaliwa kuwa kwenye maboresho.

TFF yafanya mbadiliko Ngao ya Jamii
Ligi Kuu ya NBC kuendelea leo