Aliyekua mshambuliaji wa klabu ya Chelsea Didier Drogba, amefungua milango kwa viongozi wa Olympic Marseille, kwa kuonyesha nia ya dhati ya kurejea klabuni hapo.

Drogba mwenye umri wa miaka 38, aliondoka Olympic Marseille mwaka 2004 na kuelekea Chelsea kwa ada ya Pauni milioni 24, hali ambayo iliwaacha mashabiki wa klabu hiyo katika majonzi makubwa.

Kwa sasa mshambuliaji huyo yupo huru kufuatia mkataba wake na klabu ya Montreal Impact inayoshiriki ligi ya nchini Marekani (MLS) kufikia kikomo mwishoni mwa mwaka 2016.

Drogba amesema ni wakati mzuri kwake kurejea nchini Ufaransa baada ya kuondoka kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita.

“Huenda ikawa ni taarifa ya kushtukiza kwa mashabiki wa Olympic Marseille, lakini ukweli ndio huo, japo itategemea na uongozi utakavyopokea ombi langu la kutaka kurejea nyumbani.

“Niliondoka kwa wema japo sikuwafurahisha watu wote, lakini naamini kurejea kwangu kama itawezekana inaweza kuwapa furaha nyingine mashabiki wa Olympic Marseille, ambao walionyesha simanzi wakati ninaondoka mwaka 2004.” Alisema Drogba.

Mbali na klabu ya Olympic Marseille, Montreal Impact na Chelsea Drogba pia aliwahi kuzitumikia Le Mans FC, Guingamp (Ufaransa) na Shanghai Shenhua (China).

Maalim Seif aunguruma Zanzibar,Lowassa ashukuru kwa mahaba
FC Barcelona Chupuchupu