Aliyekua nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ivory Coast Didier Drogba amejiunga na klabu ya Phoenix Rising ya nchini Marekani kama mchezaji na muwekezaji mwenza.

Drogba, mwenye umri wa miaka 39, hajacheza soka tangu mwezi Novemba mwaka jana, alipokua na klabu ya Montreal inayoshiriki ligi kuu ya soka nchini Marekani (MLS).

Klabu ya Phoenix Rising inashiriki ligi daraja la pili nchini Marekani na inatarajiwa kuwa na muonekano tofauti baada ya kufanikisha mpango wa usajili wa mshambuliaji huyo.

Inaaminiwa ujio wa Drogba klabuni hapo, huenda ukawavutia wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa kisoka duniani, hali ambayo huenda ikaiwezesha kujikongoja kutoka ligi daraja la pili na kusogea daraja la juu.

“Kumiliki sehemu ya hisa za klabu na hapo hapo kuwa mchezaji sio jambo la kawaida, lakini naamini hali hii itakua chachu kwangu dhidi ya wachezaji wengine ambao watakua wananiangalia kama kigezo chao,” Amsema Drogba.

“Ni wakati mzuri kwangu kuangalia namna ya kucheza soka na upande wa uendeshaji, naamini jambo hili litawezekana japo ninatarajia changamoto kadhaa kutoka kwa viongozi wenzangu, kocha pamoja na wachezaji.”

Hata hivyo Drogba amesema lengo lake ni kutaka kutimiza ndoto za kuwa kiongozi wa soka, na ndio maana amemua kuwa sehemu ya wamiliki wa klabu hiyo.

Amesema alijipangia atakapofikisha umri wa miaka 40 aachane rasmi na mchezo wa soka, hivyo ameona muda huo unakaribia na ndio maana amejielekeza Phoenix Rising.

Wamiliki wengine wa klabu ya Phoenix Rising ni Berke Bakay, Brett M. Johnson, Tim Riester, Diplo, Pete Wentz, Brandon McCarthy na David Rappaport.

Aliyefukuzwa Granada Kuifundisha The Desert Warriors
Serikali yamkalia kooni mkandarasi, yataka amalize ujenzi kwa wakati