Mshambuliaji mahiri wa FC Barcelona Lionel Messi huenda akawa nje ya uwanja kwa majuma matatu, kufuatia majeraha ya misuli ya paja aliyoyapata usiku wa kuamkia hii leo wakati wa mchezo wa ligi ya nchini Hispania dhidi ya Atletico Madrid.

Messi alishindwa kuendelea na mchezo huo uliounguruma kwenye uwanja wa Camp Nou, katika dakika ya 59 baada ya kupata changamoto ya kukabwa na Diego Godin.

Hii ni mara ya pili kwa mshambuliaji huyo kupata majeraha ya misuli ya paja, kwani kama itakumbukwa vyema mwanzoni mwa mwezi huu alikosa mchezo wa timu yake ya taifa ya Argentina wa kuwania kucheza fainali za kombe la dunia dhidi ya Venezuela.

Messi anatarajiwa kurejea tena uwanjani wakati wa mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Manchester City utakaopigwa Oktoba 19.

Wakati akitarajiwa kurejea katika mchezo huo, Messi atakosa nafasi ya kushiriki na wenzake katika mapambano dhidi ya Borussia Monchengladbach (Ligi ya mabingwa), Sporting Gijon na Celta Vigo (La Liga) pamoja na mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia za mwaka 2018 ambapo timu yaka ya taifa itapambana na Peru pamoja na Paraguay.

Wakati huo huo kiungo wa FC Barcelona Sergio Busquets naye alishindwa kumaliza mchezo wa jana dhidi ya Atletico Madrid kufuatia majeraha yaliyomsibu.

Video: Barcelona yaishindwa Atletico Madrid, Haya hapa magoli yote na highlights
Mourinho Na Guardiola Kukutana Tena Mwezi Oktoba