Shirikkisho la soka duniani FIFA limemtaka gwiji wa soka kutoka nchini Argentina Diego Maradona kuonesha heshima katika mchezo wa soka, na sio kuwa chanzo cha utovu wa nidhamu.

FIFA wamemtaka gwiji huyo kufanya hivyo, kufuatia ishara ya kuonyesha vidole vya kati wakati akishangilia bao la ushindi katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi kati ya Argentina na Nigeria, uliomalizika kwa taifa lake kupata ushindi wa mabao mawili kwa moja.

Mtendaji mkuu wa FIFA Colin Smith amewaambia waandhishi wa habari kuwa, wamesikitishwa na kitendo kilichoonyeshwa na gwiji huyo mwenye umri wa miaka 57, jambo ambalo amesisitiza halikua zuri kwa wanafamilia ya soka duniani.

“Haipendezi kwa mchezaji kama yeye ambaye alibahatika kuuweka mchezo wa soka katika ramani kubwa na kuandikwa vizuri katika vitabu na majarida mbalimbali, kufanya kitendo kile, hatutarajii kama kitatokea tena,” alisema Smith.

“Diego Maradona, anaendelea kuheshimika duniani kote kutokana na mazuri aliyoyafanya katika ulimwengu wa soka, hivyo hatupendi kumvunjia heshima wala yeye auvunjie heshima mchezo huu.”

FIFA wametoa muongozo huo kwa Maradona ambaye anakumbukwa kwa tukio la kufunga bao muhimu katika mchezo wa fainali za kombe la dunia mwaka 1986 dhidi ya England, kwa kutumia mkono (Mkono Wa Mungu), kutokana na kutambua homa ya pambano lijalo la Argentina dhidi ya Ufaransa huenda ikamfanya gwiji huyo atumbukie kwenye zahma ya utovu wa nidhamu.

Argentina itapambana na Ufaransa katika mchezo wa hatua ya 16 bora baadae hii leo, kwenye uwanja wa Kazan Arena, mjini Kazan

 

Ki Sung-yueng arudi ligi kuu England
Didier Deschamps ahakikishiwa usalama wa ajira