Kiungo mshambuliaji wa Simba Hassan Dilunga ‘HD’ amesema alikua na mpango wa kuikacha Simba SC, kabla ya kusaini mkataba mpya mwishoni mwa msimu uliopita.

Dilunga aliyeifungia Simba jumla ya mabao 11 tangu ajiunge nayo, yakiwamo mawili ya msimu huu na saba msimu uliopita, amesema kabla ya kusaini mkataba mpya, alikuwa amefanya mazungumzo na viongozi wa Young Africans, lakini akaamua kuwapiga chini.

Dilunga amesema: “Tulikubaliana muda wa mkataba uwe wa miaka miwili pamoja na pesa niliyotaka wanipatie waliniambia wapo tayari kunipa, lakini nilishangaa siku zinakwenda bila ya kutimiza kile tulichofikia mwisho na kukubaliana,”

“Baada ya kuona siku zinazidi kusonga mbele na hakuna lolote linalofanyika dhidi ya viongozi wa Yanga katika yale tuliyokubaliana niliona wanazingua na hawapo siriasi katika suala hilo na baada ya mabosi wangu kuniambia wapo tayari kuniongezea mkataba mpya sikuwa na hiyana.

“Nawaheshimu waajiri wangu Simba hawakutaka maneno mengi kama ilivyokuwa kwa Yanga kile tulichokubaliana na nilikuwa nahitaji katika mkataba wangu huu mpya baada ya muda mchache walilipatia na kusaini tena kwa miaka miwili nikitumikia hadi sasa.”

Amesema kilichowakwamisha Young Africans kumpa ni dau la fedha walilokubaliana, hiyo ni mara ya pili kumkosa kwani kabla ya kutua Msimbazi walitaka kumrejesha Jangwani, lakini wakazembea na kwenye Simba.

Dilunga aliwahi kuitumikia Young Africans kabla ya kwenda Stand United na kisha kurudi Mtibwa Sugar aliyoichezea mara ya mwisho 2017-2018.

Rais Samia atoa msimamo kuhusu Corona, "hatuishi kwenye kisiwa"
Manula: Simba SC ina malengo makubwa CAF